Brazil yatupa mipango ya kuandaa fainali za Kombe la Dunia soka ya wanawake 2023
Na CHRIS ADUNGO
BRAZIL imefutilia mbali mipango ya kuandaa fainali za Kombe la Dunia za soka ya wanawake mnamo 2023.
Kwa mujibu wa Shirikisho la Soka la Brazil (CBF), serikali la taifa hilo inahisi kwamba haitakuwa busara kutoa ahadi zozote za kifedha ili kufanikisha maandalizi ya fainali hizo wakati ambapo uchumi wan chi umelemazwa pakubwa na janga la corona.
Brazil kwa sasa itaunga mkono maazimio ya Colombia kupokezwa haki ya kuwa wenyeji wa kipute hicho japo watakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Japan, Australia na New Zealand ambao wamefichua azma ya kuandaa kivumbi hicho cha timu 32.
Vinara wa Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) watapiga kura mnamo Juni 25 ili kuamua mwenyeji wa fainali hizo japo Australia na New Zealand wanapigiwa upatu zaidi.
“Kutokana na athari za kiuchumi ambazo tunakabiliana nazo kwa sababu ya corona, serikali imetushauri kwamba haitakuwa vyema kutia saini mikataba inayotuweka katika ulazima wa kutimiza baadhi ya mahitaji ya Fifa ili kuwa wenyeji wa fainali zijazo za Kombe la Dunia,” ikasema sehemu ya taarifa iliyotolewa na CBF.
Brazil inajivunia kuandaa mashindano mengi ya haiba kubwa katika ulingo wa kimataifa katika miaka ya hivi karibuni, zikiwemo fainali za Kombe la Dunia za 2014, Olimpiki za 2016 jijini Rio na fainali za Copa America mnamo 2019.
Brazil imeathiriwa vibaya zaidi na ugonjwa wa Covid-19 huku zaidi ya vifo 35,000 vikiripotiwa kufikia Juni 10 na visa vya maambukizi mapya vikifikia 641,000.