Michezo

Butali, Strathmore mabingwa wa taji la Betty Tioni katika magongo

July 15th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

TIMU za Butali Warriors na Strathmore University Green zilituzwa wafalme na malkia wa magongo ya kumbukumbu za Betty Tioni baada kila moja kufanya kweli kwenye mechi zilizochezewa Uwanja wa Greensteds International School, Nakuru.

Betty Tioni aliyefariki mwaka 2017 alikuwa mchezaji wa Telkom Orange inayojivunia kubeba ubingwa wa Ligi Kuu ya mchezo huo mara 23.

Madume wa Butali Warriors ambao ndiyo mabingwa wa Ligi Kuu nchini walibeba taji hilo baada ya kulemea Holden kwa magoli 3-1 katika fainali, nao warembo wa Strathmore University Green walivuna mabao 2-0 dhidi ya USIU B.

Butali Warriors ya kocha, Dennis Owoka ilizima wapinzani wao baada ya Calvins Kanu kutikisa wavu mara mbili huku Amos Barkibir akiifungia goli moja.

Kwenye nusu fainali, Butali Warriors ilivuna ushindi wa mabao 3-0 mbele ya Strathmore University B nayo Holden iliizaba USIU Mashujaa kwa bao 1-0.

Kitengo cha wanawake, USIU B iliichapa StrathMore Orange mabao 2-1 nao wachezaji wa Strathmore Green walivuna matokeo sawa na hayo dhidi ya USIU A.

Katika robo fainali, Butali Warriors ilinyanyua FSK kwa mabao 2-1, Western Jaguars ilipigwa mabao 3-0 na Holden, Strathmore University B iliishinda Bay Club kwa goli 1-0 nayo USIU Mashujaa ilizoa mabao 2-0 dhidi ya Underdogs.