CAF: Kenya imepiga hatua maandalizi ya CHAN
SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) Jumanne lilikosa kuweka wazi utayarifu wa Kenya kwa kabumbu ya Ubingwa wa Afrika kwa wachezaji wa Ndani (CHAN 2024) hapo Agosti mwaka huu.
Wakati wa kutembelea viwanja vilivyotengewa mashindano hayo, Katibu Mkuu wa CAF Veron Mosengo-Omba alisema Kenya imepiga hatua ya maana kwenye maandalizi yake.
Hata hivyo, taifa hili litakuwa na uhakika wa kuandaa CHAN iwapo litaendelea na kasi ya maandalizi ya sasa ya kuhakikisha viwanja vyote viko tayari.
“Nilikuja hapa mnamo Desemba na hakukuwa na nyasi katika viwanja mbalimbali, leo unaweza kucheza hata gofu kwenye viwanja hivyo. Hii inaonyesha kuwa Kenya imepiga hatua kubwa na hata Nyayo imekuwa mwenyeji wa mechi mbili,” akasema Veron.
“Desemba kulikuwa na viti vichache Kasarani lakini sasa uwanja umejaa viti. Hata hivyo, kuna baadhi ya masuala ambayo lazima yakamilishwe kabla tuseme Kenya imemaliza mandalizi ya CHAN,” akaongeza.
Alikuwa akiongea kwenye afisi za wizara ya mchezo, Talanta Plaza, Nairobi akiwa ameandamana na Waziri wa Michezo Salim Mvurya, Rais wa Shirikisho la Soka Nchini Hussein Mohamed na mwenyekiti wa Kamati Andalizi ya CHAN Nicholas Musonye.
Wakati wa ziara yake, alipelekwa katika viwanja vya Kirigiti, Police Sacco, Ulinzi Sports Complex ambavyo vitatumika kwa mazoezi na timu zitakazoshiriki CHAN. Pia Veron alitembelea Kasarani na Nyayo ambazo zitatumika kuandaa mechi za CHAN.
“Hakuna aliye na uhakika kuhusu kile ambacho kitafanyika kesho lakini kutokana na kile ambacho nimekiona leo, na hatua zilizopigwa, sioni sababu ya kutocheza hapa. Hata hivyo, hilo litategemea kasi ya kuimarisha maandalizi,” akaongeza Veron.
Afisa huyo wa CAF alisema kiwango cha maandalizi Tanzania pia kinaridhisha lakini pamoja na Uganda lazima wahakikishe wanamaliza kila kitu kwa wakati.
“Iwapo eneo hili halitafanikiwa kuandaa CHAN basi itakuwa vigumu sana kuwawekea imani kuwa wataandaa Kombe la Afrika 2027,” akasema.
Mvurya naye alisema Kenya haitalegeza kamba akisema Kasarani ipo tayari kwa sababu vitu vingi vimekamilishwa na yaliyosalia ni madogo sana.
“Kile sasa tunafanya ni kuhakikisha kuwa tunaweka VAR na vifaa vingine vya kielektroniki kwa sababu lengo letu ni kuhakikisha Kenya inaandaa Afcon,” akasema Mvurya.
Waziri huyo alifichua kuwa mwanakandarasi anayefanya kazi Kasarani alilipwa Sh400 milioni mnamo Jumanne kuhakikisha anaendelea na kazi bila tatizo lolote na anakamilisha wajibu wake