Michezo

Caleb Ayodi mwenyekiti mpya wa FKF Nairobi West

November 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na JOHN KIMWERE

CALEB Ayodi Malweyi alichaguliwa mwenyekiti mpya kuongoza Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Tawi la Nairobi Magharibi baada ya kuwashinda wapinzani watatu kwenye uchaguzi uliofanyika Nyayo Stadium, Nairobi.

Caleb aliyekuwa katibu wa tawi hilo alitwaa wadhifa huo kwa kuzoa kura 38 na kuwanyoa wenzake akiwamo aliyekuwa mwenyekiti wake, Bashir Hussein aliyepata kura tano.

Caleb atasaidiana na naibu wake, Alfred Mutua Muli. Wagombeaji wengine walikuwa Charles Omondi na Simon Mugo walizoa kura sita na 14 mtawalia.

”Kwanza nashukuru wote kwa kuonyesha wana imani nami kuongoza tawi la Nairobi Magharibi kwenye juhudi za kukuza soka ndani ya miaka minne ijayo,” Caleb alisema baada ya kutangazwa mshindi.

Aidha alisema alipofikia uamuzi huo aliongea na aliyekuwa mwenyekiti wake maana katika uongozi wa soka hawastahili kuwa maadui.

Maureen Obonyo aliyechaguliwa katika wadhifa wa mwakilishi wa wanawake katika Tawi la FKF la Nairobi Magharibi. Picha/ John Kimwere

Aidha alitoa mwito kwa wenzake waliopoteza kwenye uchaguzi huo kushirikiana ili kuendeleza mchezo huo. Kadhalika alidokeza kuwa anapania kuzungumza na serikali ya Kaunti ili jitihada za kuhakikisha viwanja vya eneo vinawekwa katika hali nzuri.

Naye Hannington Khayati alichaguliwa bila kupigwa katika wadhifa wa mwakilishi wa vijana tawi hilo. Nao Maureen Obonyo na Josphat Karuri walihifadhi nyadhifa zao kama mwakilishi wa wanawake na mweka hazina.

Maureen Obonyo aliibuka mshindi kwa kukusanya kura 48 dhidi ya kura 16 zake Patricia Milimo. Pia wadau wa soka eneo hilo walionekana kuwa na imani na Karuri ambapo waliamua kumchagua kuendelea kuwabeba mkoba wa fedha katika tawi hilo. Karuri alipata kura 46 dhidi ya kura 15 za mpinzani wake, Meshack Onchonga.

Naye Charles Kaindi alichaguliwa kuhudumu katika wadhifa wa katibu alipowashinda wapinzani wake wawili.

Kaindi alichaguliwa kwa kura 43, nao Dennis Okoth na Fredrick Amoko walipata kura 15 na nne mtawalia. Kwenye uchaguzi wa mwaka 2016 mgombeaji huyo aliwania wadhifa huo lakini aliondoka mikono mitupu bila kura yoyote.A