Michezo

Chelsea yakubali ombi la Kante kutorejea kambini kwa minajili ya mechi za EPL zilizosalia msimu huu

May 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

CHELSEA wamemkubalia sogora N’Golo Kante kutojisumbua kurejea katika kambi ya mazoezi ya Cobham, Uingereza baada ya kufichua hofu ya kuambukizwa virusi vya corona.

Kocha Frank Lampard wa Chelsea pia ameshikilia kwamba kikosi chake hakitadhurika sana hata iwapo kitakosa huduma za Kante katika michuano ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) iliyosalia msimu huu.

Hata hivyo, Kante ambaye ni nyota wa zamani wa Leicester City, amehiari kujifanyia mazoezi mazito nyumbani kwake, hatua ambayo imeungwa mkono na Chelsea.

Kante alizua hofu tele miongoni mwa wachezaji wenzake wa Chelsea mnamo 2018 baada ya kuzimia akishiriki mazoezi uwanjani. Kaka yake alifariki pia kutokana na maradhi ya mshutuko wa moyo mwaka uo huo.

Kwa mujibu wa takwimu za kitaifa za wagonjwa wa corona na vifo ambavyo vinahusiana na maradhi hayo nchini Uingereza, watu weusi ndio wanaoaga dunia kwa wingi zaidi kuliko wale weupe kutokana na virusi hivyo nchini Uingereza na Wales.

Maamuzi ya Kante ya kutorejea kambini mwa minajili ya kunogesha kampeni za Chelsea katika kampeni za EPL zilizosalia muhula huu, yanajiri siku chache baada ya nahodha wa Watford, Troy Deeney kuchukua msimamo sawa na huo.

Mnamo Mei 19, 2020, vinara wa soka ya Uingereza walitangaza maambukizi sita mapya ya virusi vya corona miongoni mwa vikosi vya EPL huku kisa kimoja kikimhusisha beki matata wa Watford, Adrian Mariappa.

Chelsea kwa sasa hawajui wakati ambapo Kante, aliyekuwa sehemu ya timu ya taifa ya Ufaransa iliyojinyakulia ubingwa wa Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi, atakaporejea kambini Cobham.

Hata hivyo, wanatambua hoja ya Kante ambaye licha ya kanuni zote za afya zinazolenga kuzuia maambukizi ya corona kuzingatiwa na kila mmoja ugani Cobham na hata Stamford Bridge, hajawekewa presha ya kurejea na kambini.

Vikosi vyote 20 vya EPL vilirejea mazoeni wiki hii kwa matarajio ya kuanza upya kampeni za ligi hiyo iliyosimamishwa mnamo machi 13, kufikia Juni 12, 2020.

Hadi kusimamishwa kwa kivumbi cha EPL, Chelsea waliokuwa wamesalia na mechi tisa zaidi, walikuwa wakifunga orodha ya nne-bora jedwalini kwa alama 48.