• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 8:55 PM
Chipu yaikomoa Brazil Raga ya Dunia U-20

Chipu yaikomoa Brazil Raga ya Dunia U-20

Na GEOFFREY ANENE

KENYA iliendeleza rekodi yake nzuri dhidi ya Brazil katika raga ya wachezaji 15 kila upande hadi ushindi tatu baada ya timu yake ya chipukizi almaarufu Chipu kushinda mechi ya Kundi A 26-24 kwenye Raga ya Dunia ya daraja ya pili ya Under-20 mjini Sao Paulo usiku wa kuamkia jana.

Vijana wa kocha Paul Odera walijipata pabaya katika dakika 12 za kwanza pale walipofungwa miguso miwili kutoka kwa Dos Santos Teixeira na Leonardo De Souza. Ferrer Spago alipoteza mikwaju ya miguso hiyo.

Ikiuguza kichapo cha 63-11 kutoka kwa mabingwa wa mwaka 2008 Uruguay katika mechi ya ufunguzi Julai 9 na pia kufahamu pengine Brazil ndiyo fursa ya pekee kupata ushindi mjini Sao Paulo, Chipu ilijikakamua na kuenda mapumzikoni alama 13-10 juu.

Ilipata alama zilizoiweka mbele kupitia kwa Brian Amaitsa Masinza aliyeifungia mguso ulioandamana na mkwaju kutoka kwa nahodha msaidizi Dominic Coulson, ambaye pia alifuma penalti mbili vyema katikati ya milingoti.

Mabingwa wa Afrika Kenya walianza kipindi cha pili kwa kishindo baada ya Geoffrey Okwach kukwepa wachezaji kadhaa wa Brazil na kwa kasi ya juu, akapachika mguso chini ya milingoti na kumpa Coulson kazi rahisi ya kuongeza mkwaju.

Brazil ilifanya mabadiliko ikiingiza De Souza Oliveira katika nafasi ya Porto, lakini Kenya ndiyo ilizidi kutesa, ikiimarisha uongozi hadi 23-10 kupitia penalti ya Coulson.

Hata hivyo, mambo yalianza kuharibikia Kenya pale Brazil ilipata mguso kutoka kwa Pereira Proenca uliondamana na mkwaju kutoka kwa Spago.

Mguso mwingine kutoka kwa Ribeiro Ferreira ambao pia Spago alipachika mkwaju wake, ulipokonya Kenya uongozi, huku Brazil ikijitosa kileleni 24-23 zikisalia dakika 10 kipenga cha mwisho kilie.

“Licha ya kuwa chini mara mbili, tulijiamini na tunafurahia kupata ushindi huu,” alisema Odera baada ya mechi hiyo iliyotanguliwa na Japan kupepeta Uruguay 46-31.

Kenya, ambayo ilimaliza makala ya mwaka 2009 katika nafasi ya nne jijini Nairobi, itakamilisha mechi zake za makundi dhidi ya washindi wa mwaka 2014 na 2017 Japan hapo Julai 17. Kabla ya Chipu kupiga Brazil hapo Jumamosi, timu ya Kenya ya watu wazima almaarufu Simbas ilikuwa imechapa Brazil 27-25 katika Kombe la Emirates mjini Dubai mwaka 2011 na pia kuilima 18-17 katika mechi ya kirafiki mjini Amapa mwaka 2016.

Japan inaongoza kwa alama 10, nne mbele ya Uruguay nayo Kenya imevuna nne. Brazil iko mkiani kwa alama mbili.

Ureno na Tonga wako sako kwa bako kwa alama 10 kila mmoja kileleni mwa Kundi B baada ya kuzoa ushindi mbili kila mmoja. Canada ina alama mbili nayo Hong Kong haina kitu. Mashindano haya yatakamilika Julai 21, huku bingwa akipandishwa ngazi kushiriki Raga ya Dunia ya daraja ya juu kujaza nafasi ya Scotland iliyotemwa.

You can share this post!

AKILIMALI: Wafugaji waungana kuanzisha kiwanda chao cha...

TP Mazembe wainyeshea Atlabara 6-1 Kagame Cup

adminleo