Colombia yazima tumaini la Afrika Kombe la Dunia
Na GEOFFREY ANENE
TIMU ya mwisho ya Afrika, Senegal imeondolewa kwenye Kombe la Dunia linaloendelea nchini Urusi baada ya kuzabwa 1-0 na Colombia, Alhamisi.
Lions of Teranga ilitoshana na Japan kwa ushindi moja, sare moja na kichapo kimoja, lakini ikaaga mashindano kutokana na utovu wa nidhamu (kadi nyingi za njano kuliko Wajapani).
Vijana wa kocha Aliou Cisse walizamishwa kupitia bao la mchezaji wa Barcelona, Yerry Mina, ambaye aliruka juu na kufungia Colombia bao safi kupitia kichwa chake alipopokea kona kutoka kwa Juan Quintero dakika ya 74.
Senegal, ambayo ilihitaji sare pekee kuingia raundi ya 16-bora kutoka Kundi H, ilidhani imepata penalti katika kipindi cha kwanza baada ya Sadio Mane kuangushwa ndani ya kisanduku na beki Davinson Sanchez. Hata hivyo, baada ya refa Milorad Mazic kuangalia picha za tukio hilo kwenye video (VAR), aliamua sio penalti.
Colombia, ambayo ilianza kampeni yake kwa kubwagwa 2-1 na Japan kabla ya kushinda Poland 3-0 na kisha Senegal, imekamilisha juu ya jedwali kwa alama sita. Japan imemaliza katika nafasi ya pili kwa alama nne sawa na Senegal, huku Poland ikivuta mkia kwa alama tatu ilizopata kwa kulima Japan 1-0 katika mechi yake ya mwisho.
Senegal, ambayo iliwahi kukutana na Colombia mara mbili katika mechi za kirafiki ikipigwa 2-0 mwaka 2011 na kutoka sare ya 2-2 mwaka 2014, inaungana na Nigeria, Tunisia, Morocco na Misri kuwa shabiki.
Nigeria pia ilihitaji sare katika mechi yake ya mwisho Juni 26, lakini ikapoteza 2-1 dhidi ya Argentina. Tunisia, Morocco na Misri ziliaga mashindano mapema zilipopoteza mechi zao mbili za kwanza.