Dai vigogo Real Madrid hawana makali tena
Na MASHIRIKA
MADRID, Uhispania
KIUNGO mahiri Carlos Henrique Casemiro wa Real Madrid amekiri kwamba kikosi chao hakiko katika kiwango kizuri tangu msimu mpya utimue vumbi majuzi.
Majuzi, vigogo hao wa La Liga waliagana kwa kufungana na 2-2 na Villlarreal kutokana na mabao ya Gareth Bale.
“Itabidi sasa tuanze kupigana vikali ili tusipoteze mechi yoyote ili tusonge mbele. Upinzani ni mkali na hatupaswi kuwapa nafasi wapinzani wetu,” alisema Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 27.
Kufikia sasa, Madrid imeshinda mechi moja tu baada ya kujibwaga uwanjani mara tatu tangu pazia ya Ligi Kuu ya Uhispania ianze.
Huku akizungumzia sababu ya Bale kupigwa kadi nyekundu wakati wa mechi hiyo, kocha Zinedine Zidane alisema, licha ya raia huyo wa Wales kufunga mabao mawili, hajarejea kwenye kiwango chake bora baada ya mpango wa kujiunga na Jiangsu Suniang ya China kukwamba.
Wakati huohuo, mshambuliaji Alexis Sánchez amesema amefurahia kuondoka Manchester United na kujiunga na Inter Milan.
Raia huyo wa Chile mwenye umri wa miaka 30 amejiunga na Inter kwa mkataba wa mwaka mmoja baada ya kuifungia United mabao matano pekee katika mechi 45 msimu uliopita, licha ya kuwa ndiye aliyekuwa akilipwa pesa nyingi tangu aagane na Arsenal mnamo Januari 2018.
Akiwa na United, mshambulijai huyo amekuwa akifokewa na mashabiki baada ya kubainika kwamba alikuwa akipokea mshahara wa Sh60 milioni kwa wiki wakati hafungi mabao.
“Nilifurahia kujiunga na Manchester United kwa sababu ndio timu inayojivunia mataji mengi nchini Uingereza. Hata nilipojiunga na Arsenal pia furaha ilikuwa tele, lakini katika Manchester United lazima watu waelewe kwamba ni kikosi ambacho kilikuwa kinachengwa baada ya hadhi yake kushuka kwa kiwango fulani. Haja yangu ilikuwa kujiunga nao na kuwasaidia kushinda mataji, lakini sikufaulu. Na kamwe sitakata tamaa,” akasema.
Mabao 20
Sánchez aliifungia Arsenal mabao 80 katika mechi 166 baada ya kujiunga nao kwa kiasi cha Sh4.5 bilioni akitokea Barcelona mnamo Julai 2014, lakini kiwango chake kikashuka mara tu alipojiunga na United.
“Daima, nimekuwa nikiwaambia marafiki zangu haja yangu kuu ni kucheza soka vizuri,” Sánchez alisema.
Akasema: “Kama wangenipa fursa ya kucheza vizuri, ningecheza vizuri. Kuna wakati nilipewa muda mfupi wa kama dakika 60 kucheza, wakati mwingine ningekosa kupewa nafasi ya kucheza na sikuelewa ni kwa nini.”