David De Gea komeo namba wani anayevuna mabilioni Old Trafford
Na CHRIS ADUNGO
KIPA matata wa Manchester United na timu ya taifa ya Uhispania, David De Gea Quintana, 28, ni kati ya walinda-lango wanaodumishwa kwa mshahara mnono zaidi katika ulimwengu wa kabumbu.
Kwa sasa, ni miongoni mwa makipa wanaohemewa sana na vikosi maarufu vya bara Ulaya. Ushawishi wa De Gea kambini mwa Man-United ni kiini cha maarifa yake kuwaniwa usiku na mchana na Juventus na PSG wanaotaka abanduke ugani Old Trafford mwishoni mwa kampeni za msimu huu.
Kati ya makipa ghali zaidi ulimwenguni, De Gea anashikilia nafasi ya pili nyuma ya Manuel Neuer wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Ujerumani. Mgongo wake kimshahara unasomwa kwa karibu na Iker Casillas (FC Porto), Hugo Lloris (Tottenham Hotspur), Petr Cech (Arsenal), Jan Oblak (Atletico Madrid), Gianluigi Buffon (PSG) na Marc-Andre ter Stegen (Barcelona).
Mwezi jana, Man-United walifichua azma ya kumsajili kipa Jordan Pickford wa Everton iwapo De Gea ataagana nao. Kiini cha De Gea kutaka kubanduka ugani Trafford ni kusitasita kwa usimamizi kumpa uhakika wa nyongeza ya mshahara utakaowiana na ule wa fowadi Alexis Sanchez ambaye kwa sasa anapokea ujira wa takriban Sh42 milioni kwa wiki bila marupurupu wala bonasi.
UKWASI: Kufikia mwishoni mwa mwezi jana, majarida ya The Richest na Celebrity yalikadiria thamani ya mali ya De Gea kufikia kima cha Sh5.7 bilioni. Kiini kikubwa cha pato lake ambalo ni mshahara wa yapata Sh115 milioni ambao hupokezwa na Man-United mwishoni mwa kila mwezi. Mbali na ujira huo ambao ni zaidi ya Sh28milioni kwa wiki, De Gea hujirinia hela nyinginezo kutokana na marupurupu ya kusajili ushindi na sare katika ngazi ya klabu na timu ya taifa ya Uhispania iliyotia kapuni Kombe la Dunia mnamo 2010 na taji la Euro 2012.
Malipo hayo yanamweka De Gea ka- tika kundi moja na Romelu Lukaku, Paul Pogba na Alexis Sanchez – kikoa cha pili cha wachezaji wanaodumishwa kwa mshahara mkubwa kambini mwa Man-United ambao kwa sasa wananolewa na kocha mshikilizi mzaliwa wa Norway, Ole Gunnar Solskajer.
Kufikia sasa, wachezaji wengine wanaolipwa mshahara wa juu zaidi katika kikosi cha Man-United ni Juan Mata,
Fred, Nemanja Matic na nahodha Antonio Valencia ambaye anatarajiwa kubanduka Trafford mwishoni mwa msimu huu. De Gea pia hujipa mafungu manono ya riziki kutokana matangazo ya kibiashara anayopokezwa na kampuni mbalimbali ambazo zimemfanya kuwa balozi wa mauzo wa bidhaa zao tangu akatize rasmi uhusiano wake na Atletico Madrid mnamo 2011.
MAGARI: De Gea hana tofauti kubwa na wachezaji wa kufu yake walio na uhakika wa kutia kapuni kitita kinono cha pesa kutokana na huduma zao michumani. Ingawa anamiliki magari mengi ya haiba, mawili anayoyapenda zaidi ni Audi A6 lililomgharimu Sh12 milioni na Mercedes Benz AMG lenye thamani ya Sh18 milioni.
MAJENGO: De Gea anamiliki jumba la kifahari lenye thamani ya Sh480 milioni anakoishi jijini Manchester, Uingereza. Mbali na jengo hilo la haiba kubwa, pia ana kasri la takriban Sh220 milioni viungani mwa jiji la Madrid, Uhispania alikozaliwa.
MAPENZI NA FAMILIA: De Gea alijinasia penzi la kichuna Edurne Garcia mnamo Aprili 2014. Kipusa huyo mwenye umri wa miaka 32 kwa sasa ni mwanamitindo, mwanahabari, mwigizaji na mwanamuziki maarufu nchini Uhispania.