• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
David de Gea alegea na kukubali mabao 7 yaingie Salah akivunja rekodi ya ufungaji wa mabao katika EPL kambini mwa Liverpool

David de Gea alegea na kukubali mabao 7 yaingie Salah akivunja rekodi ya ufungaji wa mabao katika EPL kambini mwa Liverpool

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL walidhalilisha Manchester United kwa kichapo cha 7-0 ugani Anfield katika mechi iliyoshuhudia supastaa Mohamed Salah akiweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa muda wote katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kambini mwa waajiri wake.

Japo Man-United walijibwaga ugani wakijivunia ufufuo mkubwa wa makali yao chini ya kocha Erik ten Hag aliyewanyanyulia taji la Carabao Cup majuzi, Liverpool walidhihirisha ubabe wao na kuweka hai matumaini ya kukamilisha kampeni za EPL msimu huu ndani ya mduara wa nne-bora.

Liverpool walijipa udhibiti wa mechi mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya Bruno Fernandes na Marcus Rashford kupoteza nafasi za wazi za kuzamisha wenyeji wao.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool walifunga mabao yao kupitia kwa Cody Gakpo, Darwin Nunez na Mohamed Salah waliocheka na nyavu mara mbili kila mmoja kabla ya bao jingine kujazwa kimiani na Roberto Firmino.

Bao la pili la Salah lilimfanya kuwa mfungaji bora wa muda wote wa Liverpool katika EPL kwa mabao 129, moja zaidi kuliko nguli Robbie Fowler. Aidha, Salah ndiye mwanasoka wa kwanza wa Liverpool kuwahi kufunga Man-United mabao mengi zaidi (12) huku 10 kati ya magoli hayo yakitokana na mechi tano mfululizo zilizopita.

Kichapo hicho ndicho kinono zaidi kwa Liverpool kuwahi kusajili dhidi ya Man-United tangu wakomoe watani wao hao 7-1 katika Ligi ya Daraja ya Pili nchini Uingereza mnamo 1895-96.

Ushindi wa Liverpool uliweka hai matumaini yao ya kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao. Kufikia sasa, wanashikilia nafasi ya tano kwa alama 42, tatu pekee nyuma ya nambari nne Tottenham Hotspur ambao wamesakata mchuano mmoja zaidi.

Ingawa Liverpool walikomoa Man-United 5-0 ugani Old Trafford na 4-0 uwanjani Anfield katika EPL mnamo 2021-22, masogora hao wa Jurgen Klopp walitandikwa 2-1 na Man-United mwanzoni mwa msimu huu.

Katika kipindi cha siku saba, Man-United wameyeyusha ladha ya taji lao la kwanza tangu 2017 walipotandika Newcastle United na kutwaa Carabao Cup ugani Wembley.

Kichapo ambacho Man-United walipokezwa kilikuwa chao cha tatu baada ya mechi 33, kinono zaidi katika taaluma ya ukufunzi wa Ten Hag na kinono zaidi kwa masogora wake katika kipindi cha miaka 92.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

  • Tags

You can share this post!

Raila ataja mbinu mpya za kukabili serikali ya Ruto

Barcelona wakomoa Valencia na kuweka hai matumaini ya...

T L