David Rudisha nje wiki 16 baada ya upasuaji
Na GEOFFREY ANENE
MSHIKILIZI wa rekodi ya dunia ya mbio za mita 800 za wanaume, David Rudisha atakuwa mkekani kwa kati ya wiki 12 na 16 baada ya kufanyiwa upasuaji wa kifundo.
Rudisha alishindia Kenya dhahabu katika mbio hizo za mizunguko miwili katika Olimpiki 2012 mjini London nchini Uingereza kwa rekodi ya dunia ya dakika 1:40.91, hajashiriki mashindano kwa muda mrefu. Alichanika misuli mazoezini kabla ya Riadha za Dunia zilizofanyika Julai mwaka 2017 mjini London.
Mtimkaji huyo, ambaye pia anajivunia kushinda mbio za mita 800 kwenye Olimpiki 2016 mjini Rio de Janeiro nchini Brazil na mataji ya dunia mwaka 2011 mjini Daegu (Korea Kusini) na 2015 mjini Beijing (Uchina), alijeruhiwa kifundo akitembea nyumbani kwake Kilgoris katika kaunti ya Narok juma lililopita.
“Mwanzoni, Rudisha hakuamini jeraha hilo lilikuwa baya baada ya kukanyaga sehemu ya ardhi ambayo haikuwa tambarare mnamo Mei 19. Aliendelea na mazoezi akidhani hayatamletea madhara, lakini baada ya kukosa kupata afueni, alifika katika hospitali ya St Luke mjini Eldoret na ikagunduliwa kuwa alikuwa ameumia vibaya kifundo chake cha mguu wa kushoto,” Shirikisho la Riadha Duniani (WA) lilinukuu daktari Victor Bargoria akisema baada ya kumfanyia upasuaji huo hapo Mei 28.