Michezo

Dawa kusisimua misuli zamweka mwanariadha pembeni  

March 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA GEOFFREY ANENE

BINGWA wa Prague Marathon mwaka 2022 Nobert Kigen amesimamishwa kushiriki shughuli zozote za riadha hadi kesi inayomkabili ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli itasikizwa na kuamuliwa na Kitengo cha Maadili kwenye Shirikisho la Riadha Duniani (AIU).

Kigen, ambaye mashindano ya mwisho alifanya ni Xiamen Marathon nchini Uchina Januari 7, 2024, amepokea adhabu hiyo kwa tuhuma za matumizi ya dawa haramu za aina ya Testosterone.

Mtimkaji huyo mwenye umri wa miaka 31 ni Mkenya wa tano tangu Desemba 22, 2023 kuzuiwa kushiriki riadha kwa sababu ya uovu huo baada ya Sarah Chepchirchir (testosterone), Jackline Wambui (19-Norandrosterone, 19-Noretiocholanolone), mzawa wa Kenya raia wa Kazakhstan Caroline Kipkurui (kukosa kusema aliko), na Agnes Mueni Mutua (Testosterone na Trimetazidine).

Karibu wanamichezo 300 kutoka Kenya wamepokea adhabu tangu mwaka 2015 kwa matumizi ya dawa za kusisimua misuli.

Kigen alijitosa katika marathon mwaka 2015 akishinda La Rochelle Marathon nchini Ufaransa kwa muda wake bora wa saa 2:09:25. Ameshiriki marathon 10 na kutawala La Rochelle Marathon na Prague Marathon pekee.