De Bruyne kusalia Man City, Arsenal ikiendelea kumhangaikia Calafiori
KOCHA Pep Guardiola wa Manchester City amethibitisha kuwa kiungo Kevin De Bruyne hataondoka klabuni msimu huu na kuyoyomea Saudi Arabia kutafuta mihela, huku Arsenal ikikaribia kumtwaa beki mahiri, Riccardo Calafiori kutoka Italia.
Guardiola amesisitiza kwamba klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) haina mpango wa kusajili wachezaji wapya wakati huu wa usajili wa majira ya kiangazi.
De Bruyne amekuwa akiwindwa na klabu za Saudi Arabia zinazoshiriki kwenye Ligi Kuu ya Saudi Pro League, huku ikidaiwa kwamba Al-Lttihad ndio iliyokuwa na nafasi kubwa ya kumnasa staa huyo, raia wa Ubelgiji mwenye umri wa miaka 33.
“Kevin angali mchezaji wetu na hatuna mpango wa kumwachilia kwa sasa. Iwapo klabu itafanya mazungumzo na kumruhusu aondoke, tutawaelezeni kuhusu hilo, lakini hatuna mpango kama huo kwa sasa,” Guardiola aliwaambia waandishi kabla ya timu hiyo kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Celtic ugani Chapel Hill, North Carolina, jana.
“Ni kweli, hadi siku ya mwisho, tuna nafasi ya kufanya uhamisho, sikai kuwa na wachezaji wapya, lakini nadhani kuna uwezekano wa asilimia 95 kusalia kikosini, bila idadi kubwa ya wachezaji wapya kuingia. Tuna ushirikiano mzuri zaidi kikosini, huku tukitarajia mafanikio zaidi msimu ujao.”
“Kwa kweli sielewi jinsi mambo yatakavyokuwa dakika ya mwisho ukifika. Iwapo kuna mtu ataondoka, na mwingine aingie tutawaambia wakati huo,” aliongeza.
Akizungumza na waandishi wakiwa Los Angeles kwa ziara ya siku tatu ya kupimana nguvu, kocha Mikel Arteta alisema Calafiori mwenye umri wa miaka 22 kutoka klabu ya Bologna anatarajiwa kununuliwa kwa kiasi cha Sh5.8 bilioni.
“Mazungumzo yanaendelea vyema huku tukitarajia makubaliano wakati wowote,” alisema Arteta.
Kocha huyo pia ana mpango wa kuimarisha safu yake ya kiungo, baada ya ubingwa kuwaponyoka mara mbili dakika ya mwisho.
“Tunajaribu kuimarisha kikosi baada ya kumaliza nyuma ya City mara mbili mfululizo kwa tofauti ya alama chache. Tungali na muda wa kutosha kutafuta vifaa vya kuongezea kikosi nguvu ili timu iwe imara hadi dakika ya mwisho,” aliongeza.
De Bruyne aliisaidia City kutwaa ubingwa wa EPL, hii ikiwa mara ya nne mfululizo, na mara ya sita kwa jumla akichezea klabu hiyo.
Mbali na uvumi huo, vile vile kumekuwa na madai kwamba nyota Ebereche Eze wa klabu ya Crystal Palace anapanga kujiunga na Manchester City, huku mlinda lango Ederson akipanga kuyoyomea Saudi Arabia.
Manchester City, wataanza msimu kwa mechi ya EPL dhidi ya Chelsea mnamo Agosti 18, huku wakitarajiwa kukumbana na upinzani mgumu kufuatia usajili mkubwa unaofanywa na wapinzani hao wa Stamford Bridge.