Michezo

DIMBA PWANI: Wadau wa soka watamani kuona timu zaidi za Pwani zikishiriki KPL

December 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

WAKATI ambapo imebaki siku moja pekee kuukamilisha mwaka 2019, mashabiki wa kandanda wa ukanda wa Pwani wanajiuliza maswali mengi kuhusu iwapo mchezo huo umeimarika ama unaendelea kudidimia.

Washikadau kadhaa waliohojiwa na Dimba wamekuwa na maoni tofauti kuhusu hali ya kandanda katika eneo hilo ambalo awali, kulikuwa na timu nyingi zilizokuwa zikiwika kwenye Ligi Kuu ya Kenya na mashindano mengine.

Aliyekuwa kiungo wa timu iliyokuwa maarufu miaka ya kale ya Black Dragon FC, Mohamed Halwa anasema hali ya mchezo wa soka Pwani unazidi kudorora kutokana na kile anachodai kuwa ni ukosefu wa timu za kutosha katika ligi kuu.

Halwa anakumbusha kwamba wakati mmoja kulikuwa na timu nne kutoka Pwani zilizokuwa zikishiriki kwenye ligi kuu ambazo ni Mwenge, Feisal, Lake Warriors na Black Panther; wakati ambao anasema hali ya soka iliimarika mno.

“Kuwako kwa timu moja pekee ya Bandari FC katika ligi kuu, ni dhihirisho la wazi kuwa hali ya kandanda wakati huu ni duni. Ni mpaka kuweko na zaidi ya timu mbili ama tatu kwenye ligi kuu, ndipo tunaweza kujivunia kuwa Pwani imerudia hadhi yake ya zamani kisoka,” akasema.

Mmoja wa wachambuzi wa kandanda eneo la Pwani, Said Barex anasema ni sharti timu mbili za eneo hili zinazoshiriki Supaligi ya Taifa za Modern Coast Rangers FC na Coast Stima FC ziungane kupata timu moja kali ishiriki ligi kuu, bila hivyo timu hizo zitabakia hapo hapo bila kupanda ngazi.

“Tatizo tulilonalo wakati huu ni kuwa Rangers na Stima hazina wachezaji wengi wazuri na hivyo, zitabaki katika ligi hiyo daima dawamu; hakuna timu yoyote ile itakayoweza kupanda ngazi hadi ligi kuu,” akasema Barex aliyependekeza muungano wa timu hizo kupata moja kali ya Pwani.

Mchambuzi huyu alielezea masikitiko yake kuhusu timu kadhaa zilizokuwa imara na ambazo kwa wakati huu huenda zingekuwa zimepanda hadi ligi kuu kama zisingeshushwa ngazi kutokana na kushindwa kukamilisha mechi zao za supaligi ya taifa.

 

Picha ya pamoja ya klabu ya Bandari FC. Picha/ Maktaba

Akifafanua, Barex alikumbusha jinsi timu ya mtaa wa Majengo mjini Mombasa ya Admiral Youth FC ilivyokuwa ikiendelea vizuri lakini ilibidi timu hiyo iteremshwe ngazi kutokana na ukosefu wa udhamini.

“Kama Admiral ingekuwa katika ligi hiyo, ikapata udhamini, nina hakika hivi sasa tungelikuwa na timu mbili katika ligi kuu. Lakini kwa jinsi tunavyoendelea kwa sasa, hakuna matunda yoyote yatakayopatikana na Bandari itasalia kuwa timu pekee katika ligi kuu,” akasema.

Aliyekuwa meneja wa Feisal FC, Abdillahi Bashasha anasema kwamba umefika wakati kwa viongozi wa kisiasa wa Pwani wajitolee kuzisaidia timu zao zinazoshiriki kwenye ligi za taifa ili zipate kupanda hadi supaligi ya taifa na kupigania nafasi ya kushiriki ligi kuu.

“Kama timu zetu za mitaani ambazo ni za jamii hazitasaidiwa, basi soka ya eneo letu la Pwani itaendelea kudhoofika na mwishowe itazikwa kwenye kaburi la sahau,” akasema Bashasha ambaye aliwaomba viongozi kuacha kutafuta sifa za kusaidia michezo isiyohusisha Wapwani.

Kiongozi huyo alisema kati ya miradi ambayo viongozi wanapania kusaidia ni ule wa kuzawidi wanamichezo bora wa kitaifa (SOYA) na akasema pesa hizo zingetumiwa kuzifaa klabu za Pwani, basi soka ingeimarika.

Wadau wengine wa kandanda katika eneo hili wanapendekeza kuundwe kikosi cha Coast Combined FC na kishiriki Supaligi ya Taifa ili kupigania nafasi ya kupanda hadi ligi kuu. Wanaamini kwamba kikosi hicho kinaweza kushinda na kujiunga na Bandari katika ligi kuu.