• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Droo ya tenisi ya Davis Cup ya bara ni leo Jumanne

Droo ya tenisi ya Davis Cup ya bara ni leo Jumanne

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI Kenya watafahamu wapinzani wao wa mechi za makundi za mashindano ya tenisi ya wanaume ya Bara Afrika ya daraja ya tatu ya Davis Cup wakati droo itakapofanywa jijini Nairobi, leo Jumanne.

Kenya, ambayo ilishinda makala yaliyopita uwanjani Nairobi Club, itaepuka Tunisia katika mechi za makundi kutokana na kuwa timu hiyo inaorodheshwa ya kwanza katika mashindano haya nayo Kenya ni ya pili.

Timu hizi zitaunda makundi mawili ya timu nne, huku timu tatu kutoka orodha ya Algeria, Nigeria, Msumbiji, Namibia, Benin na Madagascar zikitiwa katika kundi la kwanza na zingine tatu katika kundi la pili.

Tukienda mitamboni, timu nyingi zilikuwa zimewasili katika eneo la mashindano – Nairobi Club – na hata kufanya mazoezi mle.

Tunisia, Msumbiji na Namibia zilikuwa bado hazijawasili, ingawa zilitarajiwa jijini Nairobi baadaye jana Jumatatu.

Droo itafanywa baada ya mkutano wa timu zote saa tano asubuhi.

Timu zitakazokamilisha mechi za makundi katika nafasi mbili za kwanza zitaingia katika nusu-fainali ambayo washindi watafuzu kushiriki mashindano ya daraja ya pili mwaka 2020.

Kenya itawakilishwa na wachezaji Ismael Changawa, Ibrahim Kibet, Kevin Cheruiyot, ambao walishiriki makala yaliyopita, na Albert Njogu, ambaye itakuwa mara yake ya kwanza kabisa.

You can share this post!

Ndindi Nyoro aachiliwa

KCB ni wafalme wa raga ya 7s, wajizolea Sh0.5 milioni

adminleo