Michezo

Droo ya timu za Afrika Mashariki kuchuana na Everton yatajwa

January 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

DROO ya soka ya Afrika Mashariki ya kufuzu kukutana na klabu ya Everton ya Uingereza ya SportPesa Super Cup imefanywa Jumatatu, huku mabingwa Gor Mahia wakikutanishwa na Mbao FC ya Tanzania katika mojawapo ya mechi za robo-fainali zitakazosakatwa Januari 23, 2019.

Katika makala ya mwaka huu, ambayo yanarejea Tanzania baada ya Kenya kuandaa makala ya mwaka 2018, Bandari (Kenya) itavaana na Singida United (Tanzania) katika mechi ya ufunguzi Januari 22 mjini Dar es Salaam.

Washindi wa Kombe la Ngao nchini Kenya mwaka 2015 Bandari ni moja ya timu mbili zitakazoshiriki mashindano haya kwa mara ya kwanza kabisa.

Mabingwa mara 27 wa Tanzania, Young Africans almaarufu Yanga watalimana na washindi wa Kombe la Ngao nchini Kenya mwaka 2018 Kariobangi Sharks baada tu ya Bandari na Singida kukabana koo.

Wafalme wa Kenya mara 17 Gor, ambao walishinda makala ya kwanza ya SportPesa Super Cup mwaka 2017 nchini Tanzania na kuhifadhi taji mwaka 2018, watachapana na washiriki wapya Mbao katika mechi ya kwanza ya siku ya pili.

Robo-fainali hii ya tatu itapisha mechi kati ya washindi wa Tanzania mara 19 Simba SC na mabingwa wa Kenya mara 13 AFC Leopards. Mechi za nusu-fainali ni Januari 25, huku mchuano wa kuamua nambari tatu pamoja na fainali zikisakatwa Januari 27.

Mshindi atapokea Sh3 milioni na tiketi ya kumenyana na Everton katika mechi ya kirafiki nchini Uingereza.

Gor ilibwaga Leopards 3-0 katika fainali ya mwaka 2017 na kulima Simba 2-0 mwaka 2018.