Droo ya voliboli yaepusha timu za Kenya kukutana na mabingwa watetezi Al Ahly awamu ya makundi
Na GEOFFREY ANENE
DROO ya mashindano ya voliboli ya Klabu Bingwa Afrika ya wanawake imefanywa, huku Wakenya Pipeline, Prisons na KCB wakiepuka kukutanishwa na mabingwa watetezi Al Ahly ambao pia ni wenyeji wa makala ya mwaka 2019.
Katika droo iliyofanywa na Shirikisho la Voliboli barani Afrika (CAVB), Prisons, ambao ni mabingwa wa Kenya, watalimana na Asec Mimosa (Ivory Coast), Nkumba (Uganda), GS Petroliers (Algeria) na Shams (Misri) katika Kundi D.
Prisons, ambayo inajivunia mataji ya Afrika ya mwaka 2008, 2010, 2011, 2012 na 2013, inanolewa na Josp Barasa. Warembo wa Barasa pia wanajivunia medali ya fedha mwaka 2014 walipopigwa na GS Petroliers katika fainali, na nishani ya shaba mwaka 2017.
Mabingwa wa Afrika mwaka 2006 KCB, ambao wanarejea katika mashindano ya Afrika tangu mwaka 2015, watalimana na Carthage (Tunisia) na DGSP (Congo Brazzaville) katika Kundi B. Macho yatakuwa kwa wanabenki hawa ambao mbali na kupokonya Pipeline kocha wake mkuu Japheth Munala, ambaye pia ndiye kocha mkuu wa timu ya wanawake ya Kenya, walisajili wachezaji saba wakali wa Pipeline mwezi Desemba mwaka 2018.
Mabingwa mara saba Pipeline, ambao walinyakua taji lao la mwisho mwaka 2005, wako katika Kundi C pamoja na Shooting (Misri), Revenue Authority (Rwanda) na FAP (Cameroon).
Al Ahly, ambayo inajivunia mataji mengi ya Afrika (tisa), iko katika Kundi A. Wamisri hawa wameshinda mataji matatu katika makala manne yaliyopita.
Ingawa timu 21 zilionyesha hamu ya kushiriki makala ya mwaka 2019, ni klabu 16 pekee zilipata kuingia katika droo ambayo imefanywa Ijumaa jioni mjini Cairo. Mashindano haya yanatarajiwa kuanza Machi 16 na kutamatika Machi 25.
Makundi:
Kundi A: Ahly (Misri), Customs (Nigeria), USFA (Burundi), Canon de Ndjili (DR Congo)
Kundi B: Carthage (Tunisia), DGSP (Congo Brazzaville), KCB (Kenya)
Kundi C: Pipeline (Kenya), Shooting (Misri), Revenue Authority (Rwanda), FAP (Cameroon)
Kundi D: Prisons (Kenya), Asec Mimosa (Ivory Coast), Nkumba (Uganda), GS Petroliers (Algeria), Shams (Misri)