Michezo

EPL: Nuksi ya Liverpool kuwa kileleni Krismasi kisha kulemewa kushinda ligi

January 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

MIKOSI ya Liverpool kutoshinda Ligi Kuu baada ya kuongoza Krismasi itaendelea ama itaisha msimu huu wa 2018/19?

Hili ndilo swali, wapenzi wa soka wanajiuliza zikisalia chini ya mechi 18 ligi hii ya klabu 20 itamatike.

Mashabiki wa Liverpool wana kila sababu ya kuamini itamaliza ukame wa miaka 29 bila taji ifikapo Mei 12, 2019.

Ili kutimiza ndoto yake ya kushinda Ligi Kuu kwa mara ya kwanza tangu msimu 1989/90, hata hivyo, Liverpool italazimika kukabiliana na mikosi hiyo ya kuishiwa pumzi wakati muhimu zaidi.

Baadhi ya wachezaji Liverpool itategemea kupata ufanisi ni Mmisri Mohamed Salah, raia wa Senegal Sadio Mane na Roberto Firmino, ambao wanawaka moto wakati huu. Wamechangia jumla ya mabao 28 kati ya 48 ambayo Liverpool imefunga msimu huu. Mabingwa hawa mara 18 hawajashindwa msimu huu.

Wamezoa ushindi 17 na kutoka sare mara tatu. Wameshinda mechi nane zilizopita katika mashindano yote ikiwa ni pamoja na kuaibisha Arsenal 5-1 katika mechi iliyopita. Watakuwa wakifukuzia ushindi wa 10 mfululizo ligini watakapomenyana na mabingwa watetezi Manchester City uwanjani Etihad hapo Januari 3, 2019.

Si siri mchuano huu utakuwa mtihani mgumu kwa City ambayo itapata pigo kubwa katika juhudi za kutetea taji ikipoteza. Matumaini ya Liverpool kutwaa taji yataongezeka ikivuna alama tatu dhidi ya wapinzani hawa waliowanyima taji mlangoni msimu 2013/14.

Hii hapa historia ya timu zilizoongoza Krismasi na nafasi zilizomaliza mwisho wa msimu:

Norwich iliongoza msimu wa kwanza (1992/93) wakati wa Krismasi, lakini baada ya kipenga cha mwisho iliridhika katika nafasi ya tatu nyuma ya washindi Manchester United na nambari mbili Aston Villa.

United ilihifadhi taji msimu 1993/94 baada ya kuwa juu ya jedwali wakati wa Krismasi sawa na Blackburn Rovers iliyokuwa kileleni wakati wa Krismasi msimu 1994/95 na kuushinda.

Newcastle, Liverpool, United, Aston Villa na Leeds ziliongoza wakati wa Krismasi msimu 1995/96 hadi 1999/2000, lakini hazikutwaa mataji misimu hiyo. Mataji ya msimu 1995/96, 1996/97, 1998/99 na 1999/2000 yalinyakuliwa na United nayo Arsenal ikabeba taji la msimu 1997/98. United ilijiongzea ubingwa msimu 2000/01 baada ya kuongoza Krismasi. Newcastle, Arsenal na United zilishiwa pumzi njiani misimu mitatu iliyofuata licha ya kuongoza wakati wa Krismasi. Mataji ya misimu hiyo yalinyakuliwa na Arsenal (2001/02), United (2002/03) na Arsenal ikashinda 2003/04 bila kupoteza mechi.

Chelsea ilinyakua mataji ya misimu miwili iliyofuata baada ya kushikilia nafasi ya kwanza wakati wa Krismasi. United iliongoza Krismasi na kukwamilia nafasi hiyo hadi mwisho wa msimu 2006/07. Arsenal na Liverpool hazikuwa na bahati msimu 2007/08 na 2008/09 pale zilipoongoza Krismasi, lakini mataji yaliendea United.

Chelsea, United na Manchester City ziliongoza Krismasi msimu 2009/10, 2010/11 na 2011/12 na kutwaa mataji, huku City pia ikiibuka mfalme msimu 2012/13 baada ya kuongoza Krismasi.

Nuksi ya Liverpool kutoshinda licha ya kuongoza wakati wa Krismasi ilirejea tena kuiandama msimu 2013/14 ilipomaliza nyuma ya City. Tangu msimu 2014/15, timu zote zilizoongoza wakati wa Krismasi ziliishia kukamiliosha misimu hiyo juu ya jedwali. Timu hizo ni Chelsea (2014/15), Leicester (2015/16), Chelsea (2016/17) na City ya Pep Guardiola (2017/18).