Michezo

Eto'o kubatilisha maamuzi ya kustaafu soka na kujiunga na Racing Murcia ya Uhispania

November 19th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

KIGOGO Samuel Eto’o anatarajiwa kubatilisha maamuzi yake ya kustaafu kwenye ulingo wa soka na kujiunga na kikosi cha Racing Murcia kinachoshiriki Ligi ya Daraja la Tatu nchini Uhispania.

Nyota huyo raia wa Cameroon alitangaza kustaafu soka mnamo 2019 baada ya kujivunia misimu ya kuridhisha kambini mwa Chelsea, Everton, Barcelona na Qatar SC.

Mnamo Novemba 8, 2020, Eto’o alihusika kwenye ajali ya barabarani baada ya gari alilokuwa akiendesha kugongana na jingine nchini Cameroon.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uhispania, Racing Murcia wameanzisha mazungumzo na wakala wa Eto’o kwa minajili ya kumsajili nyota huyo ambaye pia amewahi kuchezea Real Madrid, Mallorca na Inter Milan ace.

Morris Pagniello ambaye ni rais wa Murcia ameambia gazeti la Marca kwamba: “Kwa sasa tuko pua na mdomo kumsajili Eto’o. Hapo awali, matumaini yalikuwa 50-50 lakini dalili zinaashiria kwamba tunamtwaa kabla kipindi cha siku saba zijazo kukamilika.”

“Tuna wawekezaji wengi sana nchini Mexico na Falme za Kiarabu ambao wana uwezo wa kutupa fedha za kufanikisha usajili wa Eto’o. Iwapo atajiunga nasi, naamini kwamba kocha atampa nafasi ya kucheza mara kwa mara ili awe kiini cha motisha kwa chipukizi wetu wanaotazamia sana fursa hiyo,” akasema Pagniello.

Murcia wanatarajia kwamba kusajiliwa kwa Eto’o kutaweka hai matumaini yao ya kubwaga kikosi cha Levante kinachoshiriki Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwenye gozi lijalo la Copa del Rey litakalowakutanisha mnamo Disemba 16, 2020.

Murcia walijinasia huduma za kaka mkubwa wa Paul Pogba, Mathias, 30, mnamo Agosti 2020. Akivalia jezi za Barcelona, Eto’o aliwaongoza miamba hao wa Uhispania kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mara mbili kabla ya kunyanyua taji hilo kwa mara nyingine akichezea Inter Milan ya Italia.

Eto’o ambaye aliwahi kuchezea Cameroon mara 118, anajivunia kunyanyua mataji matatu ya La Liga na moja la Serie A. Alijiunga na Chelsea kutoka kambini mwa Anzhi nchini Urusi mnamo 2013. Alihudumu huko ugani Stamford Bridge kwa kipindi cha mwaka mmoja kabla ya kusajiliwa na Everton kwa miezi sita.