Michezo

Everton kuwasili nchini Julai 6 tayari kulimana na Kariobangi Sharks

July 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA mara tano wa Kombe la FA, Everton watawasili jijini Nairobi hapo Julai 6 asubuhi kwa ziara yao ya pili katika eneo la Afrika Mashariki katika kipindi cha miaka mitatu kupimana nguvu na mshindi wa soka ya SportPesa Super Cup, Kariobangi Sharks.

Vijana wa kocha Marco Silva walitembelea eneo hili mara ya kwanza katika historia yao miaka miwili iliyopita walipovaana na Gor Mahia na kuilaza 2-1 kupitia mabao ya mshambuliaji Wayne Rooney na kiungo Kieran Dowell jijini Dar es Salaam nchini Tanzania mnamo Julai 13, 2017.

 

Baadhi ya maafisa wa Everton wakiwa uwanjani Kariobangi wakiwasaidia vijana wa nyumbani kufanya mazoezi Julai 2, 2019. Picha/ Geoffrey Anene

Mvamizi kutoka Rwanda, Jacques Tuyisenge, ambaye alihama Gor mwisho wa msimu 2018-2019, ndiye alifungia mabingwa hawa mara 18 wa Kenya bao la kufutia machozi.

Timu hizi mbili zilikutana tena mwaka 2018 uwanjani Goodison Park mjini Liverpool ambapo Gor ilifanywa kitoweo kwa kumiminiwa mabao 4-0 kupitia kwa Ademola Lookman, Dowell, Nathan Broadhead na Oumar Niasse. Tuyisenge hakufanikiwa kuzuru Uingereza kwa mchuano huo kutokana na matatizo ya stakabadhi za usafiri.

Ziara ya pili ya Everton itaikutanisha dhidi ya Sharks ambayo ilipata tiketi baada ya kunyamazisha Bandari 1-0 katika makala ya tatu ya SportPesa Super Cup mnamo Januari 27 jijini Dar es Salaam.

Maafisa kadhaa wa Everton tayari wako nchini na wanaendesha vipindi vya mazoezi kwa wachezaji walio na umri tofauti tofauti kutoka mtaani Kariobangi North ilikoanzia timu ya Kariobangi Sharks miaka michache iliyopita kabla iingie Ligi Kuu msimu mwaka 2017.

Tiketi

Tiketi za mchuano huu, ambao utachezewa katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani mnamo Julai 7, zinauzwa katika sehemu mbalimbali jijini Nairobi.

Kufikia saa sita adhuhuri wenyeji Kariobangi Sharks walitangaza kuwa walikuwa wameuza tiketi 11,000.

Klabu hiyo, ambayo inanolewa na kocha William Muluya, imechapisha tiketi 60,000, ambayo ni idadi ya uwanjani wa Kasarani ukijaa kabisa.

Baadhi ya wachezaji nyota wa Everton wanaotarajiwa kuwa katika safari ya Nairobi ni Niasse (Senegal), Lookman, Calvert-Lewin (Uingereza), Mbelgiji Kevin Mirallas na Muingereza Theo Walcott.

Wakali Yerry Mina (Colombia), Richarlison (Brazil) na Yannick Bolasie (DR Congo) wanatarajiwa kukosa ziara hii kutokana na majukumu ya timu za taifa. Mina na Richarlison wamekuwa wakishiriki soka ya Amerika Kusini almaarufu Copa America nchini Brazil naye Bolasie yuko katika kikosi cha DR Congo kilicho nchini Misri kwa Kombe la Afrika (AFCON).

Mbali na mechi ya kirafiki pamoja na kufundisha wachezaji chipukizi na hata wa zamani katika uwanja wa Kariobangi Sports, maafisa wa timu hiyo pia wamekuwa wakifanya usafi katika uwanja huo.