Everton ngangari kuvaa Arsenal EPL
Na MASHIRIKA
LONDON, UINGEREZA
VITA vya kuwania nafasi ndani ya mduara wa nne-bora katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) muhula huu vitaendelezwa leo Jumapili wakati Arsenal watawaalika Everton ugani Emirates huku Manchester United wakiwavaa Watford uwanjani Old Trafford.
Katika mechi nyingine ya EPL, Norwich City wanaokokota nanga mkiani mwa jedwalini watakuwa wageni wa Wolves uwanjani Molineux. Norwich ambao wamejizolea alama 18 pekee kutokana na mechi 26 zilizopita, wana ulazima wa kuibuka na ushindi ili kukwepa shoka litakalowashusha ngazi mwishoni mwa msimu huu.
Watford nao watakuwa na kibarua kigumu cha kutia kapuni alama zote tatu ugenini ili kujiondoa katika orodha ya vikosi vinavyokodolea jicho hatari ya kuteremshwa daraja. Kikosi hicho ambacho kimepoteza jumla ya michuano 12 kati ya 26 iliyopita, kinajivunia alama 24 pekee sawa na West Ham United watakaomenyana kesho na Liverpool ugani Anfield.
Arsenal na Everton watashuka dimbani wote wakijivunia hamasa ya kusajili ushindi katika mechi zao za awali. Chini ya mkufunzi Mikel Arteta, Arsenal waliwapepeta Newcastle United 4-0 wikendi jana kupitia kwa mabao ya nahodha Pierre-Emerick Aubameyang, Nicolas Pepe, Mesut Ozil na Alexandre Lacazette wanaopigiwa upatu wa kuendeleza ushirikiano wao kwa mara nyingine Jumapili mbele ya mashabiki wa nyumbani.
Ingawa hivyo, mtihani watakaoletewa na Everton si mwepesi hasa ikizingatiwa ukubwa wa kiwango cha ufufuo wa kikosi hicho ambacho kwa sasa kinatiwa makali na kocha Carlo Ancelotti.
Ancelotti alipokezwa mikoba ya Everton mnamo Disemba 2019 baada ya kutimuliwa kwa Marco Silva aliyesajili msururu wa matokeo duni kiasi cha Everton kujipata miongoni mwa vikosi vitatu vya mwisho kufikia Novemba.
Ushindi wa 3-1 uliosajiliwa na Everton dhidi ya Crystal Palace uwanjani Goodison Park katika kivumbi kilichopita, uliwakweza hadi nafasi ya tisa jedwalini kwa alama 36, mbili zaidi kuliko Arsenal ambao wameshinda mechi saba, kuambulia sare mara 13 na kupoteza mechi sita hadi kufikia sasa ligini.
Ushindi huo ulikuwa wao wa tano mfululizo kwa Everton kupata chini ya Ancelotti anayejivunia rekodi ya kunyanyua mataji matatu ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) akidhibiti mikoba ya klabu mbili tofauti – AC Milan na Real Madrid. Kocha huyo mzawa wa Italia amewahi pia kuwanoa wanasoka wa Parma, Chelsea, Juventus, Paris Saint-Germain (PSG), Bayern Munich na Napoli.
Jumla ya alama 17 ambazo Everton wamejikusanyia tangu mwishoni mwa mwaka jana zimewaweka katika orodha ya klabu ambazo ni wagombezi halisi wa fursa ya kufuzu kwa kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.
Akihojiwa mwishoni mwa kipindi cha mazoezi ya kikosi chake mnamo Ijumaa, Ancelotti alisisitiza kwamba kubwa zaidi katika matamanio yake kwa sasa ni kuwaongoza Everton kuendeleza presha kwa Wolves, Man-United, Sheffield United, Tottenham Hotspur na Chelsea kwa matarajio kwamba wapinzani hao watajikwaa katika mechi kadhaa kati ya 12 zilizosalia ligini msimu huu.
Japo Everton wamepoteza mchuano mmoja pekee chini ya Ancelotti, ubabe wao utatiwa kwenye mizani watakaporejea ulingoni kuvaana na Man-United, Chelsea na Liverpool.