• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 12:09 PM
Everton wajitwalia huduma za kipa Olsen ili amwamshe Jordan Pickford aliyezembea langoni

Everton wajitwalia huduma za kipa Olsen ili amwamshe Jordan Pickford aliyezembea langoni

Na MASHIRIKA

EVERTON wamemsajili kipa raia wa Uswidi, Robin Olsen kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka AS Roma ya Italia.

Mlinda-lango huyo mwenye umri wa miaka 30 alihudumu kambini mwa Cagliari kwa mkopo wa mwaka mmoja mnamo 2019-20 baada ya kusajiliwa na Roma kutoka FC Copenhagen ya Denmark mnamo 2018.

Olsen anajivunia kuchezea timu ya taifa ya Uswidi mara 38 na hakufungwa bao lolote katika mechi tatu mfululizo za kufuzu kwa robo-fainali za Kombe la Dunia za 2018 nchini Urusi.

Kusajiliwa kwa Olsen kunatarajiwa sasa kutoa ushindani mkali zaidi kwa kipa chaguo la kwanza la Everton, Jordan Pickford ambaye amekuwa akifanya masihara ya mara kwa mara katika wiki za hivi majuzi.

Wiki jana, kocha Carlo Ancelotti alisema kwamba kusajiliwa kwa kipa mpya kambini mwa Everton halikuwa jambo la dharura kwa usimamizi kutekeleza. Hata hivyo, makosa mawili yaliyofanywa na mlinda-lango huyo mwenye umri wa miaka 26 yalichangia mabao mawili yalifungwa na Brighton mnamo Oktoba 3, 2020.

Hata hivyo, Everton waliibuka na ushindi wa 4-2 katika mechi hiyo iliyochezewa uwanjani Goodison Park chini ya kocha Ancelotti ambaye amechangia ufufuo mkubwa wa Everton tangu Disemba 2019.

Kabla ya kumsajili Olsen, Everton walikuwa wakihusishwa na uwezekano wa kumsajili kipa wa Manchester United, Sergio Romero na Paulo Gazzaniga wa Tottenham Hotspur.

Olsen alikuwa mchezaji wa pili kusajiliwa na Everton katika siku ya mwisho ya uhamisho wa wachezaji baada ya beki Ben Godfrey aliyejiunga nao kutoka Norwich City kwa kiasi cha Sh3.5 bilioni.

Everton ambao wamejinasia huduma za wanasoka sita muhula huu, wameagana na fowadi Sandro Ramirez ambaye ameyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Huesca kwa mkataba wa miaka mitatu.

Ramirez aliyechezea Everton mara 16 pekee na kufunga bao moja, alijiunga na Everton mnamo 2017 kwa kima cha Sh728 milioni.

Wanasoka wengine ambao wameingia katika sajili rasmi ya Evertom muhula huu ni Allan Marques, Abdoulaye Doucoure, kiungo James Rodriguez na beki wa kushoto Niels Nkounkou.

You can share this post!

Juventus wajinasia maarifa ya fowadi matata Federico Chiesa...

Wilshere afadhaishwa na hatua ya West Ham United kumtema