FARASI NI MMOJA TU! Liverpool juu mahasimu wakijikokota
Na MASHIRIKA
LEICESTER, Uingereza
LIVERPOOL imekalia kisawasawa uongozi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), baada ya kuvyoga wenyeji wake Leicester City mabao 4-0 uwanjani King Power, siku ya Alhamisi.
Mabingwa hao mara 18 wamefungua mwanya wa alama 13 juu ya jedwali, baada ya kuvuna ushindi huo muhimu kupitia mabao ya Roberto Firmino (mawili), James Milner (penalti) na Trent Alexander-Arnold.
Ulikuwa ushindi wa tisa mfululizo kwa Liverpool ligini msimu huu.
Liverpool, ambayo ilishinda taji lake la kwanza kabisa la Klabu Bingwa Duniani wikendi iliyopita nchini Qatar, sasa imepiga Leicester uwanjani King Power mara tatu mfululizo.
Vijana wa Jurgen Klopp, ambao hawajashindwa msimu huu katika ligi ya EPL, hawakuonyesha dalili za uchovu kutokana na kampeni yao katika Klabu Bingwa Duniani, wakizidia Leicester nguvu katika kila idara.
Liverpool ilikaribia kuanza maangamizi sekunde chache tu baada ya mechi kuanza, lakini kipa Kasper Schmeichel alipangua shuti kali ya beki wa kulia Alexander Arnold kutoka nje ya kisanduku.
Sekunde chache baadaye, Sadio Mane alikosa tena lango pembamba baada ya Mohamed Salah kummegea pasi safi.
Wasiwasi wa Leicester katika safu ya ulinzi ulidhihirika wazi dakika ya tano pale beki Jonny Evans alipokonywa mpira na Georginio Wijnaldum nje ya kisanduku chake, lakini Salah akapoteza nafasi nzuri baada ya kushirikiana vyema na Firmino.
Dakika sita baadaye, kasi ya kutisha na mashambulizi makali ya Liverpool yalidhihirika tena.
Reds walipata fursa ya kuvamia lango la Leicester baada ya wapinzani wao kupoteza kona.
Naby Keita alipasia Salah mpira mzuri, lakini licha ya kumchenga Schmeichel, ambaye alikuwa amelazimika kutoka nje ya kisanduku, Mmisri huyo hakuliona lango vizuri hivyo akapiga shuti yake nje ya neti.
Ngome ya Leicester ilibabaika tena na kumpatia Jordan Henderson fursa ya kumjaribu tena Schmeichel karibu na mlingoti wa kushoto.
Juhudi za Liverpool, hata hivyo, zilizaa matunda dakika ya 31.
Hatari ilioonekana ndogo wakati kona ilioondoshwa na Leicester lakini mpira ukamuangukia Alexander-Arnold nje ya kisanduku.
Beki huyo alipiga mpira safi kwa mguu wake wa kulia ndani ya kisanduku na kumpatia Firmino kazi rahisi ya kumalizia shambulio hilo kupitia kwa kichwa chake.
Vijana wa Klopp walikaribia kuimarisha uongozi huo dakika tatu baadaye wakati mhimili Virgil Van Dijk alimegea Mane pasi safi, huku raia huyo wa Senegal akijiundia nafasi nzuri ya kusukuma shuti ndani ya kisanduku.
Hata hivyo, Schmeichel alifanya kazi ya ziada kuzuia mpira kutumbukia wavuni, kwa kidari chake.
Baada ya kukosa kumjaribu kipa wa Liverpool Alisson Becker hata mara moja katika kipindi cha kwanza, Leicester ilikuwa bado na matumaini ya kurejea kwenye mechi.
Walijaribu kuongeza presha ilipogonga dakika 60. Hata hivyo, juhudi za vijana hao wa Brendan Roders zilisambaratika dakika ya 71 baada ya beki wa kati Caglar Soyuncu kunawa mpira kutokana na kona ya Alexander-Arnold.
Dakika moja baada ya kujaza nafasi ya Keita na kugusa mpira kwa mara ya kwanza, Milner alifuma wavuni penalti hiyo kwa kumbwaga kipa Schmeichel upande mmoja huku mpira ukitirika upande wa pili.
Dakika tatu baadaye, Firmino alipachika bao la tatu. Alianzisha na kisha kukamilisha shambulio hilo lililomhusisha pia Milner na Alexander-Arnold, ambaye alimega pasi safi ya mwisho.
Alexander-Arnold kisha aligonga msumari wa mwisho dakika ya 78 baada ya kupokea pasi safi kutoka kwa Mane.
Liverpool, ambayo itaalika Wolves katika mechi yake ya 19 uwanjani Anfield hapo Jumapili, sasa iko pazuri kumaliza ukame wa karibu miaka 30 bila taji la Ligi Kuu EPL.
Leicester itazuru West Ham ugani London Stadium ikilenga kumaliza mechi tatu bila ushindi.