Michezo

Fataki zatarajiwa Diamond League Chepkoech na Chespol wakisaka ushindi

June 10th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

 

Na GEOFFREY ANENE

ITAKUWA fataki katika mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji kwenye duru ya tano ya Riadha za Diamond League ambazo zimevutia washikilizi wa rekodi ya dunia Beatrice Chepkoech (watu wazima) na Celliphine Chespol (Under-20) jijini Olso nchini Norway hapo Juni 13, 2019. Orodha ya washiriki imetangazwa Jumatatu.

Chepkoech alitimka rekodi ya dunia ya dakika 8:44.32 mjini Monaco mwaka 2018 naye Chespol aliweka rekodi ya dunia ya chipukizi ya dakika 8:58.78 nchini Marekani mwaka 2017.

Bingwa wa Afrika mwaka 2018 Chepkoech na mshindi wa dunia kwa wakimbiaji wasiozidi umri wa miaka 20 mwaka 2018 Chespol ni baadhi ya talanta ya hali ya juu iliyoingia duru ya Oslo.

Wakali wengine kutoka Kenya watakaonogesha jijini Oslo ni mshindi wa Afrika mwaka 2016 Norah Jeruto (8:59.62), bingwa wa dunia mwaka 2015 Hyvin Kiyeng (9:00.01), mshindi wa Olimpiki ya chipukizi Fancy Cherono (9:31.00) na bingwa wa dunia wa chipukizi mwaka 2006 Caroline Tuigong (9:28.81).

Wakimbiaji 17 watashindania taji katika kitengo hiki ambacho Kenya inapigiwa upatu kung’ara. Hata hivyo, ushindani mkali unatarajiwa kutoka kwa Mwamerika Emma Coburn (9:02.58), Mjerumani Gesa Felicitas Krause (9:11.85) na Mganda Peruth Chemtai (9:17.78).

Aidha, Kenya itakuwa na mwakilishi mmoja pekee katika mbio za mita 800 ambapo Cornelius Tuwei atawania ubingwa dhidi ya wakimbiaji wengine wanane kutoka mataifa ya Puerto Rico, Australia, Norway, Ireland, Uswidi na Poland. Tuwei anajivunia muda bora wa dakika 1:44:91 katika mbio hizi za mizunguko miwili.

Raia wa Puerto Rico Ryan Sanchez na Andres Arroyo ni wakimbiaji wengine waliotimka umbali huo chini ya dakika 1:45 msimu huu waliongia duru hii. Sanchez amekamilisha umbali huu kwa dakika 1:44:82 naye Arroyo (1:44.96).

Nao Wakenya Paul Tanui, Davis Kiplangat na Cornelius Kangogo watajaribu bahati yao katika mbio za mita 3,000 ambazo zimevutia watimkaji 15 wakiwemo mfalme wa Jumuiya ya Madola wa mbio za mita 5,000 na mita 10, 000, Joshua Cheptegei (Uganda) na Waethiopia Muktar Edris na Selemon Barega.

Kitengo kingine ambacho Wakenya wameingia jijini Olso ni mbio za kilomita 1.6 (maili moja). Hapa kunao Justus Soget, Vincent Kibet na Bethwell Birgen. Watapata mtihani mkali kutoka kwa ndugu Filip Ingebrigtsen na Jakob Ingebrigtsen (Norway), Ayanleh Souleiman (Djibouti) na Muethiopia Aman Wote.

Wakenya walifanya vibaya katika duru iliyopita jijini Rome nchini Italia mnamo Juni 6. Walimaliza nje ya nafasi tatu za kwanza katika mbio walizoshiriki za mita 800 na mita 5000 (wanaume) na mita 1500 (wanawake), huku Benjamin Kigen akiondolea Kenya aibu kwa kutwaa taji la mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na maji. Duru ya sita itaandaliwa mjini Rabat nchini Morocco mnamo Juni 16. Mashindano yote yanajumuisha duru 14.