Michezo

Fifa yapendekeza timu ziruhusiwe kubadilisha wachezaji watano badala ya watatu katika kila mechi

April 28th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Soka Duniani (FIFA) limependekezea klabu kuchezesha hadi wachezaji watano wa akiba katika hatua ambayo inatarajiwa kuleta nafuu ya kumudu mrundiko wa mechi baada ya ligi mbalimbali kurejelewa.

Ligi Kuu mbalimbali za soka zimesimamishwa kote duniani kutokana na janga la virusi vya homa kali ya corona.

Pendekezo la FIFA huenda likatekelezwa kwa michuano yote ambayo imeratibiwa kuchezwa hadi mwishoni mwa msimu wa 2021.

“Afya huja mwanzo. Hakuna mashindano yoyote ambayo yanastahili kuhatarisha maisha ya binadamu hata mmoja,” ikatanguliza sehemu ya taarifa iliyotolewa na FIFA.

“Vipute vya soka vinastahili tu kurejelewa baada ya wasimamizi wa masuala ya afya na maafisa wa serikali kuwahakikishia wadau wote usalama wao.”

“Usalama wa wachezaji ni miongoni mwa majukumu makuu ya FIFA. Hatari tunayotazamia pindi baada ya ligi mbalimbali kurejelewa ni matukio ambapo baadhi ya wanasoka watawajibishwa katika mechi nyingi kupita kiasi. Matokeo yake ni majeraha mengi mabaya ya mara kwa mara,” ikasisitiza taarifa hiyo.

Pendekezo la FIFA linatazamiwa kuidhinishwa na Bodi ya Kimataifa ya Mashirikisho ya Soka (IFAB) ambayo ina majukumu ya kubuni kanuni na sheria za mchezo wa soka.

Hata hivyo, FIFA imesisitiza kwamba utekelezaji wa kanuni hiyo, iwapo itaidhinishwa na IFAB, kutasalia kuwa maamuzi ya mashirikisho binafsi baada ya kushauriana na wadau wengine katika viwango vyao.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uingereza, vinara wa IFAB wanatarajiwa kuwa wepesi wa kuidhinisha pendekezo hilo la FIFA kwa kuwa ni suala lililowahi kujadiliwa kwa kina na kuafikiwa kuwa mojawapo ya njia kuu zinazoashiria kwamba maslahi ya wachezaji yanazingatiwa ipasavyo.

Kanuni itakavyofanya kazi

  • katika mashindano ambapo kwa sasa wachezaji wasiozidi watano wa akiba wanakubaliwa kuchezeshwa, vikosi vitakuwa na fursa ya kuchezesha hadi wanasoka watano wa akiba katika mechi moja
  • kati ya wachezaji wote watano wa akiba, ni watatu pekee watakaokubaliwa kuingia uwanjani katika nyakati tofauti tofauti za mchezo isipokuwa mwishoni mwa kipindi cha kwanza.
  • mchezaji wa sita wa akiba huenda akaruhusiwa kuwajibishwa uwanjani wakati wa kipindi cha ziada; yaani baada ya muda wa dakika 90 za kawaida za mchezo kukamilika na mechi kuingia katika dakika 30 za ziada
  • kanuni hii mpya itatekelezwa tu katika kiwango cha timu za taifa kwa mechi zitakazokuwa zimeratibiwa kusakatwa hadi Disemba 31, 2021.