Michezo

FKF yataka wizara iruhusu Harambee Stars kuanza mazoezi kwa minajili ya mechi dhidi ya Zambia na Comoros

September 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Soka la Kenya (FKF) limetuma maombi kwa Wizara ya Michezo kukubali kurejelewa kwa mchezo wa soka humu nchini.

Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF, Barry Otieno, amethibitisha kuandikwa kwa barua rasmi ambayo imetumwa kwa wizara hiyo inayoongozwa na Waziri Amina Mohamed.

“Kenya imepangiwa kushiriki mechi ya kirafiki dhidi ya Zambia mwezi Oktoba jijini Nairobi. Tunahitaji kujiandaa kwa mechi hiyo vilivyo. Tumeomba Wizara ya Michezo itukubalie kuita wachezaji kambini na kuanza maandalizi kwa wakati ufaao,” akasema Otieno.

“Gor Mahia pia wana kibarua katika soka ya Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) na tunahitaji kupata mshindi wa FKF Shield Cup ili tupate mwakilishi wa Kombe la Mshirikisho barani Afrika (CAF Conferations Cup) msimu huu wa 2020-21.

“Katika barua yetu kwa Wizara ya Michezo, tumeahidi kwamba wanasoka watazingatia kanuni zilizopo za kudhibiti msambao wa virusi vya corona na tutazidi kuwakumbusha wadau wote husika,” akaongeza Otieno.

FKF imeandikia pia klabu zinazochezewa na wanasoka wa Harambee Stars katika mataifa ya ughaibuni ziwaachilie wachezaji hao kusafiri humu nchini pindi kocha Francis Kimanzi atakapowaita kambini kwa minajili ya mechi ya kirafiki dhidi ya Zambia.

Baada ya kupimana nguvu na Zambia, Stars wamepangiwa kupiga mechi za mikondo miwili za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021 dhidi ya Comoros mnamo Novemba 2020.

Kati ya wanasoka wanaotarajiwa na Kimanzi kuvalia jezi za Stars kwa mara ya kwanza katika vipute hivyo ni beki wa kushoto wa Barnsley, Clarke Oduor.

Masogora wa Kimanzi wamepangiwa kushuka dimbani kuvaana na Comoros katika mechi za Kundi G za kufuzu kwa AFCON 2021 mnamo Novemba 9 nyumbani kisha Novemba 12 ugenini.

Ni matumaini ya Kimanzi pia kwamba vijana wake, hasa wanaosakata soka ya humu nchini, watapata fursa ya kujiandaa mapema kabla ya kushiriki michuano hiyo mitatu katika kipindi cha miezi miwili ijayo.

Kocha huyo aliyewaongoza Mathare United kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mnamo 2008, ameridhishwa mno na tukio la Stars kupanda kwa nafasi moja zaidi kutoka nambari 107 hadi 106 kwenye orodha ya viwango bora vya kimataifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka Duniani (Fifa) mnamo Septemba 17.

“Hizi ni habari za kutia moyo sana hasa ikizingatiwa kwamba hatujashiriki mchuano wowote kwa miezi kadhaa iliyopita. Sasa tuna changamoto kubwa ya kujitahidi hata zaidi kuimarika kwenye orodha hiyo. Tulifanya vyema kabla ya mkurupuko wa virusi vya corona.”

Stars kwa sasa inashikilia nafasi ya pili kwenye Kundi G la kufuzu kwa fainali za AFCON 2021.

Stars wanajivunia alama mbili kutokana na sare za 1-1 dhidi ya Misri ugenini mnamo Novemba 14, 2019 na Togo nyumbani mnamo Novemba 19, 2019 katika mechi mbili za ufunguzi wa Kundi G.