Michezo

Fulham yamezea mate huduma za Divock Origi

January 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MBELGIJI Divock Origi anamezewa mate na klabu ya Fulham, ripoti nchini Uingereza zinasema.

Mshambuliaji huyu wa Liverpool, ambaye wazazi wake ni Wakenya, hajaridhisha uwanjani Anfield tangu anunuliwe kutoka klabu ya Lille nchini Ufaransa kwa Sh1.3 bilioni Julai 29, 2014. Alirejeshwa katika klabu ya Lille kwa mkopo baada tu ya kununuliwa na kuisakatia msimu 2014-2015.

Alichezea Liverpool msimu 2015-2016 kabla ya kupelekwa Wolfsburg nchini Ujerumani kwa mkopo msimu 2017-2018.

Alirejea Liverpool msimu huu wa 2018-2019 na kuifungia bao muhimu lililozamisha majirani wao Everton 1-0 kwenye Ligi Kuu mnamo Desemba 2, 2018 kipa Jordan Pickford alipofanya masihara.

Tetesi sasa zinasema kwamba kocha mkuu wa Fulham, Claudio Ranieri ameahidiwa fedha na viongozi wa klabu hiyo ili aimrishe kikosi chake mwezi huu wa Januari timu hiyo inapotafuta kujinasua kutoka mduara hatari wa kutemwa.

Fulham ilitumia Sh13 bilioni katika kipindi kirefu cha uhamisho kilichopita baada yua kurejea Ligi Kuu, lakini mambo hayajaiendea vyema. Inashikilia nafasi ya 19 kwenye ligi hii ya klabu 20 baada ya kuzoa alama 14 kutokana na mechi 21 ilizosakata. Timu tatu za mwisho hutupwa katika Ligi ya Draja ya Pili.

Fulham inatamani sana kuwa ikifunga mabao, na Origi, kulingana na vyombo vya habari nchini Uingereza, ataipa makali yanayokosekana katika safu ya mbele, ambayo imemtegemea sana Aleksandar Mitrovic.

Inasemekana kwamba Fulham iko tayari kuipa Liverpool karibu Sh2 bilioni ili ipate huduma za Origi, ambaye ana umri wa miaka 23.