Michezo

Ghana yazimia Kenya ndoto ya kufuzu magongo Olimpiki

August 12th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imepata pigo katika juhudi zake za kurejea katika Olimpiki kwenye fani ya mpira wa magongo ya wanaume baada ya kutupa uongozi mara mbili na kulazwa 3-2 na Ghana katika mchujo wa Bara Afrika ulioanza mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini mnamo Agosti 12, 2019.

Vijana wa kocha Meshack Senge, ambao walichabanga Ghana 4-3 mara ya mwisho walikuwa wamekutana katika mashindano haya mwaka 2015, waliongoza 1-0 wakati wa mapumziko kupitia bao la Constant Wakhura lililopatikana dakika ya 28.

Ghana ilisawazisha katika robo ya tatu 1-1 kupitia kwa Benjamin Kwofie kabla ya Kenya kuchukua uongozi tena 2-1 katika robo ya mwisho kupitia kwa Festus Onyango dakika ya 51. Hata hivyo, Ghana ilikuwa na mipango tofauti na kusawazisha tena 2-2 kupitia kwa Akaba Elikem dakika moja baadaye na kisha kufuma wavuni bao la ushindi kupitia kwa Salya Nsalbini sekunde ya mwisho kutokana na kona fupi.

Kenya ilishiriki Olimpiki mwaka 1956, 1960, 1964, 1968, 1972, 1984 na 1988. Imekuwa ikijitahidi kurejea katika Olimpiki, lakini bila mafanikio. Mwanzo mbaya katika mashindano ya kuingia Olimpiki mwaka 2020 inaiweka pabaya zaidi kwa sababu mchujo huu unatumia mfumo wa mzungumzo.

Mechi hii ilitanguliwa na Misri kuaibisha Zimbabwe 6-0 kupitia mabao ya Ahmed Elganaini (matatu), Amr Sayed (mawili) na Amr Ibrahim (moja).

Kenya itamenyana na Misri katika mechi yake ijayo mnamo Agosti 13, Ghana ilimane na Namibia nayo Afrika Kusini ikabane koo na Zimbabwe siku iyo hiyo. Vijana wa Senge watapambana na Zimbabwe (Agosti 15), Afrika Kusini (Agosti 17) na kukamilisha mchujo huo dhidi ya Namibia mnamo Agosti 18.

Mshindi pekee ndiye atajikatia tiketi ya kushindan nchini Japan mwaka ujao. Tausi, ambayo ni timu ya wanawake ya Kenya, ilianza kampeni yake kwa kulemea Namibia 1-0 kupitia bao la Grace Makokha. Kinadada wa Kenya hawajawahi kushiriki Olimpiki katika mpira wa magongo. Watakuwa na kibarua kigumu zaidi katika mechi yao ijayo dhidi ya Ghana mnamo Agosti 13 kabla ya kulimana na Zimbabwe (Agosti 15) na Afrika Kusini (Agosti 17).