Gichu: Mipango yote ya kura ya Gor imekamilishwa
MWENYEKITI wa Bodi ya Uchaguzi wa Gor Mahia Gichu Wahome Ijumaa, Aprili 11, 2025 alisema kuwa mipango yote imekamilishwa kuelekea kura ya klabu itakayoandaliwa uwanja wa Nyayo mnamo Jumapili.
Hii ni baada ya Jopo la Kutatua Mizozo ya Michezo (SDT) kuamrisha kuwa wawaniaji ambao walikuwa wamefungiwa nje waruhusiwe kuwania kura hiyo.
Waliofungiwa nje ni Mwekahazina wa sasa Dolphina Odhiambo na aliyekuwa mwekahazina wa awali Sally Bollo. Odhiambo anawania uenyekiti wa klabu hiyo huku Bollo akilenga wadhifa wa naibu mwenyekiti.
“Tulipata uamuzi wa SDT na majina ya wale ambao walikuwa wameachwa nje yamejumuishwa. Tumeshauriana na IEBC kuhusu hilo na sasa kilichosalia ni wanachama wapige kura kuwachagua viongozi wao,” akasema Wahome kwenye mahojiano na Taifa Dijitali.
“Wale ambao walikuwa wamelipa ada za awali ambazo zilikuwa juu, watarejeshewa sehemu ya pesa zao lakini mikakati yote ya kiusalama inasalia ile ile na nina hakika kura hiyo itafanyika kwa njia ya amani,” akaongeza.
Odhiambo mwenyewe alisema kuwa sasa ameridhishwa na maandalizi na yupo tayari kumenyana na Ambrose Rachier katika kuendea uenyekiti wa Gor Mahia.
Alithibitisha kuwa amelipa ada ambazo zinahitajika na akashukuru SDT kwa kuwafanyia haki wagombeaji ambao walikuwa wamefungiwa nje.
Awali, bodi ya kura ya Gor ilikuwa imeweka Sh500, 000 na Sh450, 000 kwa wanaowania uenyekiti na naibu mwenyekiti lakini SDT ikashusha kiwango hicho hadi Sh150, 000 na Sh100, 000 mtawalia.
Jumla ya mashabiki 1992 wa Gor watashiriki kura hiyo ambapo iwapo Rachier atashinda, basi atakuwa akihudumu muhula wake wa mwisho baada ya kuongoza Gor tangu 2009.