Gor kusaka nyota wa kigeni kuijaza nafasi ya Tuyisenge
Na CHRIS ADUNGO
MWENYEKITI wa Gor Mahia, Ambrose Rachier amesisitiza kuwa itawalazimu kumsaka nyota wa kigeni atakayejaza nafasi ya Jacques Tuyisenge haraka iwezekanavyo.
Hii ni licha ya Paul Were wa Harambee Stars ambaye amepania kutorefusha mkataba wake kambini mwa AFC Leopards kuhusishwa na uwezekano wa kutua kambini mwa Gor Mahia.
Tuyisenge ambaye ni mzawa wa Rwanda yuko pua na mdomo kuingia katika sajili rasmi ya Petro Atletico nchini Angola.
Kulingana na Rachier, usimamizi wa Gor tayari unalenga kuanzisha mazungumzo na wachezaji wawili wa kigeni kwa matarajio kwamba mmoja wao atahiari kujiunga nao.
“Tutamwendea mchezaji wa haiba kubwa kutoka nje ya nchi iwapo Gor itaafikiana na Petro ambao tayari wamewasilisha ombi la kutaka kujivunia huduma za Tuyisenge msimu ujao,” akatanguliza.
“Hatutaki kabisa kulijaza pengo la Tuyisenge kwa kutumia mchezaji mwingine wa KPL.
Tunawafuatilia masogora wawili tunaohisi wana uwezo wa kuziba kwa mafanikio pengo litakalosalia,” akaongeza.
Mbali na Petro ambao wako radhi kuweka mezani kima cha Sh15 milioni, vikosi vingine vinavyoyahemea maarifa ya Tuyisenge ni AS Vita kutoka DR Congo na miamba wawili wa soka ya Tanzania – Simba SC na Yanga.
“Kwa sasa tunatathmini ofa mbalimbali kutoka kwa klabu zinazowania huduma za Tuyisenge. Sioni tukifaulu kumzuia nyota huyo kuyoyomea popote atakapo,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia, Lordvick Aduda.
Tuyisenge alisajiliwa na Gor miaka mitatu iliyopita katika uhamisho uliogharimu kiasi cha Sh4 milioni zilizomchochea kubanduka kambini mwa Police FC nchini Rwanda.
Wengine
Zaidi ya Tuyisenge, wachezaji wengine ambao huenda wakaagana na Gor ni nahodha Harun Shakava, beki Philemon Otieno na kiungo Francis Kahata, 28.
Shakava anahusishwa pakubwa na vikosi mbalimbali kutoka Zambia na Simba SC ambao wapo radhi kutoana jasho na CS Constantine ya Algeria ili kujitwalia ubunifu wa Kahata. Otieno anaviziwa sana na Black Leopards ambayo kwa sasa inanolewa na kocha wa zamani wa Gor, Dylan Kerr nchini Afrika Kusini.