• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 9:35 PM
Tuyisenge amezewa mate na klabu kadha

Tuyisenge amezewa mate na klabu kadha

Na GEOFFREY ANENE

MVAMIZI matata wa Gor Mahia na taifa la Rwanda, Jacques Tuyisenge anamezewa mate na klabu kadhaa barani Ulaya, tetesi zinasema.

Kwa mujibu wa tovuti ya michezo ya Transfermarkt, Tuyisenge, ambaye ni nahodha wa timu ya taifa ya Rwanda, alinunuliwa na mabingwa hawa mara 17 wa Kenya mnamo Februari 1 mwaka 2016 kutoka klabu ya Police Kibungo kwa ada ya uhamisho ya Sh4,764,923.

Mchezaji huyu aliyezaliwa Septemba 22 mwaka 1991 amekuwa akifanya vyema tangu awasili. Katika msimu wake wa kwanza, Tuyisenge alifungia Gor mabao 10 ligini na kumaliza katika nafasi ya nne nyuma ya Wakenya John Mwakata (15), Wycilffe Ochomo (12) na Kepha Aswani (11).

Alikamilisha katika nafasi ya tatu kwa magoli 13 katika ligi ya mwaka 2017, huku Masoud Juma na Meddie Kagere wakishikilia nafasi mbili za kwanza kwa kucheka na nyavu mara 17 na 14, mtawalia.

Mwaka 2018, Tuyisenge alimaliza katika nafasi ya pili kwa pamoja na Elvis Rupia baada ya kutikisa nyavu mara 15. Eric Kapaito aliibuka mfungaji bora baada ya kufungia Kariobangi Sharks mabao 16.

Tuyisenge amefikisha magoli matatu katika mechi 15 ambazo Gor imesakata ligini.

Hata hivyo, ameonyesha ukatili wake mbele ya goli katika mashindano ya klabu ya Afrika.

Mechi tano

Amefunga katika mechi tano mfululizo hii ikiwa ni bao moja dhidi ya Lobi Stars ya Nigeria (Desemba 16, 2018), bao moja dhidia ya New Star kutoka Cameroon (Januari 13, 2019), mabao mawili dhidi ya Zamalek ya Misri (Februari 3, 2019), bao moja dhidi ya Hussein Dey ya Algeria (Februari 24, 2019) na bao moja dhidi ya Petro de Luanda ya Angola (Machi 17, 2019).

Kasi yake ya kutisha, ‘jicho la goli’ pamoja na ustadi wake wa kufuma penalti zimefanya avutie klabu za kigeni.

Kabla ya ripoti kuibuka Ijumaa kwamba anamezewa mate na klabu kutoka Bara Ulaya zikiwemo kutoka nchini Cyprus anakotoka kocha mku wa Gor, Hassan Oktay, klabu ya AS Vita kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilisemekana ina hamu kubwa naye.

Inaaminika Vita inataka kufufua mipango yake ya kusajili Tuyisenge, ambaye sasa Oktay ameshauri Gor imemuongeze kandarasi na kuimarisha mshahara wake ili asiwazie kuondoka. 

  • Tags

You can share this post!

KIPWANI: Hana choyo, kizuri anakula na chipukizi

Serikali yalenga kuangamiza TB ifikapo 2025

adminleo