Michezo

Gor Mahia kwenye mizani ya Green Eagles ya Zambia

July 17th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Hassan Oktay wa Gor Mahia amewaonya wachezaji wake dhidi ya utepetevu watakaposhuka leo Jumatano dimbani kuvaana na Green Eagles ya Zambia katika robo-fainali ya kipute cha kuwania ubingwa wa Cecafa Kagame Cup.

Gor Mahia ambao ni mabingwa mara 18 wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL), walikamilisha kampeni zao za Kundi D kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo (KMKM) kutoka Zanzibar mwishoni mwa wiki jana.

Wakipania kutia kapuni taji la kivumbi hicho kinachodhaminiwa na Rais wa Rwanda Paul Kagame, Gor Mahia walianza kampeni zao kwa kuwachabanga AS Maniema kutoka DR Congo 2-1 kisha kupepeta AS Ports ya Djibouti 2-0 katika mechi ya pili.

Licha ya ufanisi huo uliwapa Gor Mahia fursa ya kutawala kilele cha kundi lao, Oktay ameonya kwamba Green Eagles ambao wamepumzika kwa takriban siku tano, watapania kujituma zaidi wakifahamu ukubwa wa uwezo wa wapinzani wao.

“Mambo ni mazuri kufikia sasa. Kosa kubwa litakalofanywa na Gor Mahia ni kuingia katika mechi ya leo wakiwabeza wapinzani hasa baada ya kujivunia matokeo ya kuridhisha katika hatua ya makundi,” akaonya Oktay.

Maniema waliokamilisha mechi za Kundi D katika nafasi ya pili kwa alama sita baada ya kulaza Ports 2-1, watachuana na APR FC ya Rwanda katika robo-fainali nyingine ya leo Jumatano.

TP Mazembe

Jumanne ilikuwa zamu ya TP Mazembe kutoka DR Congo kuvaana na mabingwa watetezi wa Kagame Cup, Azam FC kutoka Tanzania huku wenyeji Rayon Sport wakichuana na KCCA ya Uganda.

Maniema ilikuwa timu ya mwisho kutinga hatua ya robo-fainali mnamo Jumapili baada ya kuwalabua Ports kupitia kwa mabao ya wachezaji Kilangalanga Pame na Lutonadio Tegi.

kunako dakika za 10 na 13 mtawalia. Ports ambao pia wangefuzu wangewacharaza Maniema, walifungiwa bao la kufutia machozi na Gabriel Dadzie katika dakika ya 71.

Mazembe ambao ni mabingwa mara tano wa soka ya Afrika, ni wamealikwa katika kivumbi cha Cecafa mwaka 2019.

Waliingia hatua ya robo-fainali baada ya kupepeta KMC kutoka Tanzania 1-0 na kuwazamisha Atlabara kutoka Sudan Kusini 6-1.

Mechi za nusu-fainali zitasakatwa mnamo Ijumaa ya Julai 19 huku fainali ikitandazwa Julai 21.