Michezo

Gor Mahia wajiandaa kwa kivumbi na Nzoia Sugar leo Jumatano

October 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MABINGWA mara 18 na washikilizi wa taji la Ligi Kuu ya Kenya (KPL), Gor Mahia wameratibiwa leo Jumatano kuvaana na Nzoia Sugar katika kivumbi kitakachotandazwa ugani Mumias Sports Complex.

Gor Mahia waliobanduliwa na USM Alger ya Algeria kwenye kipute cha Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) wikendi iliyopita, watakuwa wakilenga sasa kuendeleza ubabe wao katika KPL kwa matumaini ya kutetea ufalme na kutia kapuni taji la 19.

Mchuano wa leo unawapa jukwaa mwafaka la kutafuta ushindi wa nne mfululizo mbele ya mashabiki wa nyumbani wa Nzoia Sugar ambao wameapa kulipiza kisasi.

Timu hizi zilipokutana ligini kwa mara ya mwisho mnamo Mei 15, 2019, Gor Mahia walisajili ushindi mwembamba wa 1-0 mjini Mumias.

Gor Mahia watajibwaga ugani wakijivunia nafasi ya nane jedwalini kwa alama sita walizozipata kwa kuwaponda mabingwa mara 11 wa KPL, Tusker FC 5-2 na wanabenki wa KCB 2-1 katika michuano miwili ya ufunguzi wa kampeni za muhula huu.

Ushindi kwa Gor Mahia ambao kwa sasa wananolewa na mkufunzi Steven Polack utawashuhudia wakichupa hadi kileleni mwa jedwali la ligi hii ya klabu 18.

Ingawa hivyo, uongozi wao kileleni huenda ukadumu kwa kipindi cha saa chache tu iwapo Bandari FC watawapepeta wageni wao Posta Rangers katika kivumbi cha kesho kitakachowakutanisha uwanjani Mbaraki Sports, Mombasa.

Chini ya mkufunzi Bernard Mwalala, Bandari wanashikilia nafasi ya sita kwa alama saba sawa na Kakamega Homeboyz, Ulinzi Stars, KCB, Tusker na mabingwa mara 13 wa KPL, AFC Leopards.

Kwa sasa, wanaumeme wa Western Stima wako juu kwa alama nane kutokana na ushindi mara mbili na sare mbili. Kubanduliwa kwa Gor Mahia kwenye CAF Champions League kunawasasa katika ulazima wa kushiriki kivumbi cha Kombe la Mashirikisho la Afrika.

Ingawa hivyo, watahitajika kushinda mmoja wa washindi 16 wa raundi ya kwanza ya mashindano hayo ya daraja ya pili ili kufuzu kwa mechi za hatua ya makundi.

Baadhi ya timu zilizoshinda mechi za raundi ya kwanza ya Kombe la Mashirikisho ni RS Berkane, Hassania Agadir (Morocco), Zanaco (Zambia), ESAE (Benin), DC Motema Pembe (DR Congo), Bidvest Wits, TS Galaxy (Afrika Kusini), Proline (Uganda) na Triangle United (Zimbabwe).

Gor Mahia pia walishiriki Kombe la Mashirikisho msimu uliopita baada ya kubanduliwa nje ya Klabu Bingwa katika raundi ya kwanza. Waliondoa New Star ya Cameroon katika mechi ya kutafuta tiketi ya kushiriki mechi za makundi kwa jumla ya mabao 2-1 na kufika robo-fainali kutoka kundi lililojumuisha Zamalek (Misri), Hussein Dey (Algeria) na Petro de Luanda (Angola).

Hata hivyo, walidhalilishwa na Berkane kwa jumla ya mabao 7-1 katika robo-fainali baada ya kupokezwa kichapo cha 2-0 uwanjani MISC Kasarani na 5-1 nchini Morocco mnamo Aprili mwaka huu.