Michezo

Gor ndio 'dawa' ya timu za Kiarabu, wasema mashabiki

February 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA GEOFFREY ANENE

Baada ya kuufanya uwanja wa Kasarani kuwa kichinjio kwa klabu za Zamalek kutoka Misri na Hussein Dey ya Algeria, mashabiki wa Gor Mahia sasa wanaamini klabu yao ni ‘dawa’ ya Waarabu.

Wakizungumzia ushindi wa mabao mawili bila jibu dhidi ya Dey mnamo Jumapili, mashabiki wa Gor wanaofahamika kwa jina la utani kama Green Army, wamemiminia sifa tele mabingwa hawa wa Kenya.

Shabiki Abiud Oluoch anasema, “Hongera (Gor Mahia)! Tunajivunia sana kazi yenu. Nyinyi ndiyo dawa ya Waarabu.”

Kiungo Francis Kahata na mshambuliaji Jacques Tuyisenge walihakikishia Gor ushindi muhimu dhidi ya Dey ambao umewafanya kuondoa Waalgeria hawa juu ya Kundi D katika soka ya Kombe la Mashirikisho la Afrika.

Vijana wa Hassan Oktay walipoteza nafasi chungu nzima kabla ya Kahata kutikisa nyavu za Dey katika dakika ya 83 kupitia shuti kali kutoka kwa mguu wake wa kulia baada ya kipa Gaya Merbah kutema krosi hatari kutoka pembeni kushoto.

Merbah, ambaye aliponea mara kuadhibiwa katika kipindi cha kwanza kwa kutematema mipira, hakuwa na jibu alipobaki pekee yake na Tuyisenge katika dakika ya 88 baada ya Mrwanda huyo kupata walinzi wa Dey wamezembea.

Gor ilinufaika pakubwa kupata bao la pili Dey iliposalia wachezaji 10 uwanjani baada ya Chamseddine Harrag kuonyeshwa kadi yake ya pili ya njano katika mechi hiyo.

Mabingwa hawa mara 17 wa Kenya sasa wana alama sita kutokana na mechi tatu. Wataalikwa na Dey nchini Algeria katika mechi ijayo mnamo Machi 3 siku ambayo Petro de Luanda pia ikimenyana na Zamalek kutoka Misri nchini Angola.

Gor kabla ya kukamilisha mechi za makundi kwa kukaribisha Petro uwanjani Kasarani mnamo Machi 17. Vijana wa Oktay walilima Zamalek 4-2 jijini Nairobi na kulemewa 2-1 na Petro jijini Angola mapema mwezi huu.

Vikosi vya Gor na Hussein Dey (wachezaji 11 wa kwanza):

Gor – Bonface Oluoch, Harun Shakava, Charles Momanyi, Philemon Otieno, Kenneth Muguna, Samuel Onyango, Lawrence Juma, Nicholas Kipkurui, Shafik Batambuze, Francis Kahata, Jacques Tuyisenge; Hussein

Dey – Gaya Merbah, Walid Alati, Tougai Mohamed, Abdelghani Khiat, Naoufel Khacef, Mehdi Ouertani, Hocine El Orfi, Chamseddine Harrag, Ahmed Gasmi, Faouzi Yaya, Ilyes Yaiche.