Gor yaadhibu Homeboyz na kukaribia taji la 17 KPL
Na GEOFFREY ANENE
MIAMBA Gor Mahia sasa wanahitaji alama nane kutoka michuano yao tisa iliyobaki kujishindia taji la 17 la Ligi Kuu baada ya kulipua Kakamega Homeboyz 3-1 mjini Kisumu, Jumatatu.
Mabao kutoka kwa Innocent Simiyu dakika ya 31, raia wa Burundi Francis Mustapha dakika ya 34 na Kevin Omondi dakika 89 yamesaidia vijana wa kocha Dylan Kerr kudumisha rekodi ya kutoshindwa na Homeboyz hadi mechi nane ligini na kufungua mwanya wa alama 14 juu ya jedwali la ligi hii ya klabu 18.
Gor, ambayo inatafuta taji la pili mfululizo, imezoa alama 62 kutokana na mechi 25. Itatawazwa bingwa ikishinda mechi tatu zijazo dhidi ya Chemelil Sugar (Agosti 16), mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka (Agosti 22) na mahasimu wa tangu jadi AFC Leopards (Agosti 25).
Mabingwa wa Kombe la Ngao mwaka 2015 Bandari wanashikilia nafasi ya pili kwa alama 48. Bandari wamesakata mechi 27. Wanafuatiwa na Leopards (45), Sofapaka (43), mabingwa mara nne Ulinzi Stars (38) na washindi wa mwaka 2008 Mathare United (38), ambao wamecheza mechi 26 kila mmoja na wanao uwezo mdogo wa kutwaa taji ikiwa watashinda mechi zao zote na Gor wapoteze vibaya mechi zao zote zilizosalia.
Mabingwa mara 11 Tusker pamoja na Kariobangi Sharks, washindi wa mwaka 2006 SoNy Sugar, na Homeboyz wanafunga 10-bora kwa alama 36, 34, 33 na 33, mtawalia.
Nafasi nne zinazofuata zinashikiliwa na Zoo Kericho (alama 32), Posta Rangers (31), Nzoia Sugar (30) na Nakumatt (29). Timu katika hatari zaidi ya kutemwa ni Chemelil Sugar (alama 27), Vihiga United (26), Wazito (23) na Thika United, ambayo inavuta mkia kwa alama 20.