Michezo

Gor yajiandaa kupiga mechi 8 Agosti

July 31st, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na CECIL ODONGO

MABINGWA mara 16 wa ligi kuu nchini KPL, Gor Mahia  watawajibikia mechi nane za KPL mwezi Agosti kama njia ya kupunguza msongamano  katika ratiba yao mkondo wa pili wa ligi unapoendelea.

Kulingana na ratiba mpya iliyotolewa kwa timu hiyo, K’Ogalo pia watacheza mechi mbili za mashindano ya Bara ya Afrika za kuwania ubingwa wa kombe la mashirikisho, CAF ndani ya mwezi uo  huo.

Gor watawakaribisha Rayon Sports kutoka Rwanda ugani Kasarani kwa mechi ya CAF Agosti 19 kabla ya kusafiri hadi Algeria  Agosti 29 kuhitimisha mechi za kundi hilo kwa kucheza dhidi USM Algiers.

Mabingwa hao watetezi ambao walirejea nchini Jumatatu Agosti 30 kutoka Tanzania walikowakalifisha Yanga SC mabao 3-2 katika mechi hiyo  ya CAF watajibwaga uwanjani Jumatano Agosti 1 kuanza kuwajibikia ratiba hiyo ngumu kwa kushiriki mechi ya KPL dhidi ya Kariobangi Sharks uwanjani Moi jijini Kisumu.

Jumamosi Agosti 4 Mibabe hao watavaana na Nakumatt FC mjini  Machakos, siku tatu baadaye watifue vumbi dhidi ya  Bandari mjini Mombasa na hatimaye wahitimishe wiki hiyo kwa kidumbwedumbe dhidi ya Posta Rangers.

Mechi kubwa ya mkondo wa pili ya debi ya Mashemeji kati ya Gor Mahia na AFC Leopards inayosubiriwa kwa hamu na hamumu imeratibishwa kuchezwa Agosti 25 katika uwanja wa Kasarani.

Gor Mahia v K. Sharks – Kisumu (Agosti 1), Nakumatt v Gor Mahia – Machakos (Agosti 4), Bandari v Gor Mahia – Mombasa (Agosti 7), Posta Rangers v Gor Mahia – Narok (Agosti 10), Gor Mahia v Kakamega Homeboyz – Machakos (Agosti 13), Gor Mahia v Chemelil – Machakos (Agosti 16), Gor Mahia v Rayon – Kasarani (Agosti 19), Sofapaka v Gor Mahia – Narok (Agosti 22), Gor Mahia v Leopards – Kasarani (Agosti 25) na USM Alger v Gor Mahia – Algeria (Agosti 29).