Gor yasagwasagwa na Berkane na kufunganya virago soka ya CAF
Na GEOFFREY ANENE
MABINGWA wa Kenya, Gor Mahia wanatarajiwa kurejea nchini leo Jumanne usiku baada ya kampeni yao ya kusonga mbele kwenye Kombe la Mashirikisho la Afrika kufika ukingoni ilipochapwa 5-1 na Berkane nchini Morocco na kuaga kipute hicho kwa kuzidiwa maarifa kwa jumla ya mabao 7-1, Jumapili.
Safari ya Gor katika mashindano ya soka ya Afrika msimu 2018-2019 ilianza Novemba 28 mwaka 2018 katika mechi za kuingia raundi ya kwanza ya Klabu Bingwa na kutamatika katika robo-fainali ya Kombe la Mashirikisho hapo Aprili 14, 2019.
Gor ilitua nchini Morocco kwa mechi ya marudiano saa chache kabla ya mechi baada ya kukumbwa na masaibu mengi yaliyoilazimu kusafari kwa vikundi viwili kutokana na kuchelewa kupata tiketi za kusafaria.
Kocha Hassan Oktay amenukuliwa nchini Morocco akitetea wachezaji wake dhidi ya kipigo hicho akisema anajivunia kazi yao hasa kwa sababu ilifanywa katika hali ngumu baada ya vituko vingi kushuhudiwa katika safari yao.
Vituko hivyo vilianzia jijini Nairobi pale timu hiyo ilichelewa kusafiri baada ya Wizara ya Michezo kukosa kutoa tiketi za ndege mapema.
Vilichangia Gor kukosa kulala ama kulala katika sakafu ya uwanja wa ndege jijini Doha nchini Qatar na pia wachezaji kuwa na uchovu.
Kundi la mwisho la wachezaji wa Gor liliwasili uwanjani saa mbili kabla ya mechi baada ya kusafiri karibu kilomita 800 kutoka mji wa Casablanca hadi Berkane.
Ombi lakataliwa
Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) pia lilikataa ombi la Gor kutaka kuahirishwa mechi hiyo iliyopangiwa kuanza saa nne usiku kwa saa chache ama siku.
Mashabiki pia wametetea wachezaji na kusema walijaribu kadri ya uwezo wao katika hali hiyo ngumu.
Lawama kubwa ya mashabiki imeelekezwa kwa viongozi wa Gor wakisema hawajui wanachofanya ofisini na kuwataka wajiuzulu mara moja.
Wameshambulia uongozi wa Ambrose Rachier wakisema ulishindwa kufanya mipango mizuri ya usafiri.
Baada ya kuchapwa na Berkane, Gor sasa imesalia kushindania Ligi Kuu pekee.
Ilibanduliwa nje ya soka ya SportPesa Shield ilipolemewa na Bandari majuzi.