GSU, KCB mabingwa wa voliboli Arthur Odera
Na JOHN KIMWERE
TIMU za Kenya General Service Unit (GSU) na KCB zilifanikiwa kutwaa taji la Arthur Odera Open Volleyball kitengo cha wanaume na wanawake mtawalia zilipolemea wapinzani wao katika fainali zilizoandaliwa mjini Malaba, Kaunti ya Busia.
Wafalme wa mchezo huo nchini, GSU ilituzwa kombe la kipute hicho ilipopepeta mahasimu wao Halmashauri ya Bandari ya Kenya (KPA) kwa seti 3-2 kwenye mechi iliyoshuhudia ushindani mkali.
Wanaume hao wanaopania kuhifadhi ubingwa wa Ligi Kuu KVF kwa mara ya pili mfululizo walilemea wenzao kwa alama 25-22, 25-21,19-25,26-28,15-12.
Nao warembo wa KCB ambao hutiwa makali na kocha, Japheth Munala alivishwa umalkia wa ngarambe hiyo waliangusha malkia wa zamani, Kenya Pipeline kwa seti 3-0 (25-20, 25-20,25-20).
Naibu wa kocha wa KCB, David Kinga alisema “Bila shaka matokeo ya kikosi chetu yaonyesha kimejipanga imara kuvuruga mahasimu wao kwenye kampeni za Ligi Kuu ya KVF muhula huu.”
Kwenye nusu fainali GSU ilikomoa Bungoma County kwa seti 3-0 (25-15, 25-16,25-12) nayo KPA ilizoa seti 3-1(25-19, 25-19, 24-26, 25-14) dhidi ya Equity Bank. Nao vipusa wa KCB walinyorosha Bungoma County kwa seti 3-0 (25-13, 25-12, 25-12), huku Kenya Pipeline ikiandikisha seti 3-0 (25-22, 25-17, 25-15) mbele ya DCI.
Kwa wanawake kipute hicho kilijumuisha timu kama:Juja, Kahawa Barracks, Huruma Queens, Busia Divas na Sky Hawk kati ya zingine.