Guardiola asajili beki chipukizi wa Peru
Na CHRIS ADUNGO
MANCHESTER City wameafikiana na kikosi cha Alianza Lima kinachoshiriki Ligi Kuu ya Peru kuhusu uhamisho wa beki chipukizi Kluiverth Aguilar hadi uwanjani Etihad.
Hata hivyo, Aguilar ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya Peru, atasalia kambini mwa Lima hadi Mei 2021 atakapohitimu umri wa miaka 18 ndiposa aanze kuvalia rasmi jezi za Man-City.
Kwa mujibu wa maafisa wa Man-City, Aguilar ambaye ni beki wa kulia yuko tayari kuanza kuchezea Lima kwa mkopo hadi umri wake utakapomwezesha kupata kibali cha kufanyia kazi nje ya Peru na hususan Uingereza.
Uhamisho wa Aguilar umeelezwa na kikosi cha Lima kuwa ndio “mkubwa na muhimu zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya soka ya Peru katika kipindi cha miaka michache iliyopita”.
“Ni tija na fahari tele kuwa mchezaji wa kwanza wa Peru katika miaka ya hivi karibuni kuwahi kuingia katika sajili rasmi ya kikosi kinachoshiriki soka ya bara Ulaya. Kubwa zaidi katika maazimio yangu ni kuendelea kujitahidi kwa matumaini ya kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Man-City katika siku zijazo,” akasema Aguilar.
Aguilar aliwajibishwa kwa mara ya kwanza na timu yake ya taifa mnamo Novemba 2019 baada ya kuteuliwa kuunga kikosi cha kwanza cha wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 katika kampeni za kuwania ufalme wa soka ya Amerika Kusini. Alikuwa na umri wa miaka 15 pekee wakati huo.