Michezo

GUMZO LA SPOTI: Napoli yalima Liverpool huku Lyon wakiwacharaza Arsenal

July 30th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

EDINBURGH, SCOTLAND

NAPOLI iliwapokeza Liverpool kichapo kinono cha 3-0 siku saba kabla ya miamba hao wa soka ya Uingereza na Bara Ulaya kushuka dimbani kuvaana na Manchester City katika kivumbi cha kuwania taji la Community Shield.

Kwingineko, Moussa Dembele alitokea benchi na kufunga mabao mawili katika ushindi wa 2-1 uliosajiliwa na Lyon dhidi ya Arsenal katika fainali ya Emirates Cup.

Mchuano huo uliwapa Gabriel Martinelli na Dani Ceballos jukwaa la kuwawajibikia Arsenal kwa mara ya kwanza tangu wasajiliwe msimu huu. Bao la pekee la Arsenal lilifumwa wavuni na Pierre-Emerick Aubameyang katika dakika ya 36.

Kocha Unai Emery hakuwachezesha Mesut Ozil na Sead Kolasinac katika mchuano huo ikizingatiwa mkasa wao wa kushambuliwa na watu waliojihami kwa kisu.

Lorenzo Insigne alihusika katika mabao yote matatu ya Napoli katika mchuano huo uliosakatwa mnamo Jumapili ugani Murrayfield, Scotland.

Mechi hiyo ilikuwa ya nne kwa Liverpool ya kocha Jurgen Klopp kupiga bila ya kusajili ushindi kadri inapojifua kwa kampeni za msimu mpya.

Insigne aliwafungulia Napoli ukurasa wa mabao kunako dakika ya 17 kabla ya kushirikiana vilivyo na Arkadiusz Milik aliyepachika wavuni goli la pili katika dakika ya 28.

Kombora lililovurumishwa na Insigne langoni pa Liverpool lilimrudia mshambuliaji Amin Younes aliyezamisha kabisa chombo cha wapinzani wao baada ya kutemwa na kipa Simon Mignolet kunako dakika ya 52.

Kipute hicho kilitoa jukwaa kwa Liverpool kumwajibisha chipukizi Harvey Elliott waliomsajili kutoka Fulham mapema Jumapili.

Kusuasua kwa mabeki wa Liverpool uliwashuhudia wakifungwa mabao mawili ya haraka chini ya dakika 30 licha ya kujivunia wachezaji saba kati ya 11 waliounga kikosi cha kwanza kilichowapepeta Tottenham Hotspur kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu jana.

Katika mechi hiyo, Liverpool ilikosa huduma za kipa Alisson Becker na wavamizi Roberto Firmino, Mohamed Salah na Sadio Mane.

Wanne hao hawajashiriki mchuano wowote wa kujipima nguvu kufikia sasa kwa sababu ya majukumu yao ya hivi karibuni katika timu zao za taifa.

Tegemeo

Alisson na Firmino walitegemewa sana na Brazil katika kivumbi cha Copa America huku Salah na Mane wakiwajibishwa na mataifa yao ya Misri na Senegal kwenye fainali za Kombe la Afrika (AFCON).

Wanapojiandaa kuvaana na Man-City wikendi hii ugani Wembley, kiungo Georgino Wijnaldum amekiri kwamba hali ya Salah, Mane, Firmino na Alisson ni suala ambalo linawakosesha usingizi.

Liverpool na Man-City ndivyo vikosi vilivyojizolea alama nyingi zaidi katika kampeni za EPL msimu uliopita.

Wakijivunia huduma za mafowadi matata zaidi, City walitikisa nyavu za wapinzani wao mara 169 katika mashindano yote huku saba kati ya wachezaji wao wa kikosi cha kwanza wakifunga zaidi ya mabao 10 kila mmoja. Ingawa Liverpool nao walitia fora, ni wachezaji wao watatu pekee ambao walipachika wavuni zaidi ya mabao saba.

Baada ya kuchuana na Man-City katika Community Shield, Liverpool ambao ni washikilizi wa taji la UEFA, watafungua kampeni za EPL dhidi ya Norwich City kisha wamenyane na Chelsea katika Uefa Super Cup.

Hii itakuwa mechi yao ya tatu chini ya siku tisa.

City wanaolenga ubingwa wa EPL kwa mwaka wa tatu mfululizo, pia wanakosa huduma za wanasoka mahiri katika kikosi chao kinachojiandaa kwa muhula ujao.

Gabriel Jesus alikuwa na Firmino katika kikosi kimoja cha Brazil huku Sergio Aguero na Riyad Mahrez wakiwachezea Argentina na Algeria kwenye fainali za Copa na AFCON mtawalia.

Ingawa hivyo, wingi wa mafowadi kambini mwa City unamweka kocha Pep Guardiola katika ulazima wa kutegemea huduma za Raheem Sterling, Phil Foden, Bernardo Silva na Leroy Sane anayewaniwa kwa sasa na Bayern Munich.