• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:15 PM
Haaland abeba Dortmund na kuweka historia ya ufungaji katika UEFA

Haaland abeba Dortmund na kuweka historia ya ufungaji katika UEFA

Na MASHIRIKA

ERLING Braut Haaland wa Borussia Dortmund alifunga mara mbili dhidi ya Club Bruges ya Ubelgiji na kuweka historia ya kuwa mchezaji aliyepachika wavuni mabao 15 ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) haraka zaidi.

Chipukizi huyo raia wa Norway aliwafungulia Dortmund ukurasa wa mabao katika dakika ya 18 baada ya kushirikiana vilivyo na kiungo mvamizi Jadon Sancho aliyefunga bao la pili la waajiri wake kabla ya Haaland, 20, kucheka na nyavu kwa mara nyingine kunako dakika ya 60.

Haaland ambaye ni miongoni mwa masogora wanaoinukia kwa kasi zaidi katika ulingo wa soka ya bara Ulaya, alifikisha jumla ya mabao 15 ya UEFA kapuni mwake baada ya mechi 12 pekee, saba chini ya idadi ya michuano ambayo vigogo wastaafu Ruud van Nistelrooy na Roberto Soldado walihitaji katika enzi zao za uchezaji.

Dortmund kwa sasa wanahitaji alam moja pekee kutokana na mechi mbili zijazo za makundi ili kujikatia tiketi ya hatua ya 16-bora ya UEFA kutoka Kundi F. Hata hivyo, ushindi katika mchuao ujao dhidi ya Lazio utawapa tiketi ya kushiriki mechi za mwondoano.

Haaland aliyetawazwa Chipukizi Bora wa Mwaka wa 2020 kwa kutwaa tuzo ya Golden Boy alikuwa mchezaji wa pili baada ya Didier Drogba kufunga mabao matano ya UEFA kwa haraka zaidi alipochukua michuano mitatu pekee kufikia hatua hiyo.

Chipukizi huyo alihitaji mechi saba pekee kufikisha idadi ya mabao 10 katika soka hiyo ya bara Ulaya.

Idadi kubwa zaidi ya mabao ambayo yalikuwa yamefungwa na mchezaji mmoja katika UEFA baada ya mechi 12 pekee ni magoli 11 yaliyofumwa wavuni na mshambuliaji wa zamani wa timu ya taifa ya Brazil, Adriano.

Sancho ambaye makali yake yamepungua pakubwa tangu aanze kuhusishwa na uwezekano wa kutua kambini mwa Manchester United msimu uliopita wa 2019-20, aliachwa kwenye benchi wakati wa mchuano wa Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) uliokutanisha Dortmund na Hertha Berlin wikendi iliyopita.

You can share this post!

KMPDU yamlaumu Kagwe kwa kudai madaktari wanapata corona...

Neymar afunga penalti dhidi ya RB Leipzig na kumpunguzia...