HAENDI: Arsenal yakaribia kukamilisha mazungumzo na Bukayo Saka
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
ARSENAL wanakaribia kukamilisha mazungumzo ya kumnasa kinda Bukayo Saka kwa mkataba wa muda mrefu ambao utatangazwa rasmi juma hili.
Saka ambaye ni kinda kutoka katika kituo cha Arsenal cha kunoa vipaji, amekuwa mchezaji tegemeo katika kikosi cha kocha Mikel Arteta msimu huu wa 2019-20, hata baada ya kuchezeshwa katika nafasi tofauti kikosini.
Tangu msimu urejelewe baada ya miezi mitatu, Arsenal imecheza mechi nne katika muda usiozidi siku 11 ambapo kinda huyo amekuwa akipewa nafasi kutokana na mbinu zake za hali ya juu.
Alicheza kama beki wa kushoto kwenye pambano la majuzi ambapo Arsenal waliibuka na ushindi wa 2-0 dhidi ya Southampton ugani St Mary’s.
Katika pambano jingine la Kombe la FA, kinda huyo alicheza kama kiungo mshambuliaji akishirikiana na Alexandre Lacazette na Nicolas Pépé.
“Mazungumzo kati ya familia na wakuu wa klabu yamekuwa yakiandelea vyema kwa miezi kadhaa iliyopita,” kocha Arteta alisema kabla ya kikosi chake kukutana na Southampton katika ligi kuu ya EPL majuzi.
“Ni mchezaji mwenye bidii anayependa kuimarika kila wakati.”
Kulingana na David Ornstein wa Atletico Madrid, Arsenal pia wamezidisha kampeni za kumnasa kiungo Thomas Partey, 27 raia wa Ghana.
Kwingineko, klabu ya Leicester City inatarajia kuchezea nyumbani mechi zake tatu za Ligi Kuu (EPL) zilizobakia licha ya jiji hilo kufungwa kutokana na uongezeko na mambukizi ya corona.
Klabu hiyo inashauriana na baraza la jiji hilo, kundi moja la ushauri wa kiusalama pamoja na wakuu wa Ligi Kuu (EPL) na hivyo basi imetangaza mikakati madhubuti ya usafi na usalama katika kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo.
Msemaji wa Leicester alisema, “Makundi yote husika yameridhika, kupitia kwa mikatati ya kupambana na Covid-19, klabu inaweza kuendelea kuendesha shughuli zake chini ya masharti yaliyowekwa, huku tukiamini kwamba hakutatokea madhara yoyote kwa wachezaji wake, wale wa timu ngeni pamoja na jamii zilizo karibu na jiji hili. “Kwa sasa, mazoezi yetu yataendelea katika uwanja wa Belvoir Drive, huku mechi zetu za nyumbani zikibakia jinsi zilivyopangwa.”
Katika ratiba hiyo, Leicester City maarufu kama Foxes wamepangiwa kukutana na Crystal Palace kabla ya kuvaana na Sheffield United na baadaye Manchester United, katika juhudi za kutafuta kumaliza katika nne bora na kufuzu kwa soka ya Klabu Bingwa barani Ulaya.
Sekta ya afya jijini hapa iliamuru Jumanne maduka ya rejareja yafungwe baada ya visa vya corona kuenea katika muda wa wiki moja iliyopita.
Leroy Sane
Wakati huo huo, klabu ya Manchester City imekubaliana na Bayern Munich kuhusu nyota Leroy Sane kwa mkataba utakaogharimu Sh5.5 bilioni.
Sane amekuwa akihusishwa na mpango wa kujiunga na Bayern Munich lakini mpango huo ulivurugwa na jeraha.
Lakini kocha wake, Pep Guardiola amethibitisha kwamba makubaliano yameafikiwa kwamba staa huyo ajiunge na vigogo hao wa Bundesliga baada ya mkataba wake kumalizika mwishoni mwa msimu huu.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa timu ya Ujerumani anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka mitano na mabingwa hao wa Ligi Kuu ya Ujerumani.