Hakuna mgawanyiko kati ya wachezaji au klabu – Messi
Na MASHIRIKA
BARCELONA, Uhispania
LIONEL Messi alisisitiza Jumatano kuwa hakuna uhasama kati yake na Antoine Griezmann ama mgawanyiko kati ya wachezaji na viongozi wa klabu ya Barcelona.
Messi alianza mechi yake ya pili msimu huu baada ya kutoka mkekani dhidi ya Inter Milan katika michuano ya Klabu Bingwa Ulaya, huku timu yake ya Barca ikitoka nyuma bao moja na kulima Waitaliano hao 2-1 uwanjani Camp Nou.
Katika mahojiano baada ya mechi, Messi aliulizwa kuhusu uhusiano wake na Griezmann, ambaye Jumanne alikiri kuwa alipata ugumu kushirikiana na raia huyo wa Argentina alipokuwa akiuguza jeraha.
“Bila shaka, hatuna tatizo,” alisema Messi, ambaye aliibuka mwanasoka bora wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) wa mwaka 2019 zaidi ya wiki moja iliyopita.
Aliongeza: “Kuna uhusiano mzuri baina yetu, sisi ni kitu kimoja. Tulihitaji ushindi huu na sasa tunatumai tutaendelea kuwa katili kutoka hapa.”
Mshambuliaji wa Uruguay, Luis Suarez alifungia Barcelona mabao mawili, bao la pili likipatikana dakika ya 85 alipomegewa pasi safi kutoka kwa Messi. Barcelona sasa inatoshana na Borussia Dortmund kwa alama nne juu ya jedwali la Kundi F.
Madai pia yaliibuka kuwa kuna mgawanyiko kati ya wachezaji wa Barcelona na viongozi wa klabu hiyo, huku Gerard Pique akidokeza kuwa taarifa zilizochapishwa wikendi iliyopita zikikosoa timu zilitoka kwa maafisa wa ngazi ya juu ya klabu hiyo, ingawa Messi alipuuzilia mbali kuwa uhusiano umezorota.
“Tuko sawa. Kitu muhimu ni kuzungumzia ushindi ambao tumepata leo (Jumatano) na mechi yetu ijayo dhidi ya Getafe. Tutamenyana na Sevilla kabla ya kipindi cha mechi za timu za taifa. Tutajaribu kupata alama zote tatu kwa sababu inasababisha hali ya kutokuelewana. Tutalenga kukamilisha kipindi hiki vyema kabla ya kujiunga na timu zetu za taifa,” alisema.
Kipa amwagwa
Inter ilitangulia kuona lango mapema baada ya Lautaro Martinez kucheka na nyavu za Barca dakika ya pili.
Alipokea pasi nzuri kutoka kwa Alexis Sanchez na kumwaga kipa Marc-Andre ter Stegen.
Martinez alipata fursa ya kuimarisha uongozi wa Inter dakika ya 16, lakini hakudhibiti mpira vyema na kupatia mabeki wa Barca nafasi ya kuondosha hatari. Kabla ya nusu saa, Antonio Candreva alifungia Inter bao la pili, lakini hata hakusherehekea kwa sababu alikuwa amerombeza.
Inter, ambayo ilikosa huduma za mvamizi matata Romelu Lukaku kutokana na jeraha, ilipoteza nafasi mbili nzuri kutoka kwa Martinez na Sanchez kabla ya mapumiziko na kuishia kujuta. Suarez alisawazisha 1-1 dakika ya 58 alipomegewa pasi murwa kutoka kwa Arturo Vidal kabla ya kupachika bao la ushindi zikisalia dakika tano mechi kukatika. Barcelona sasa haijapoteza mechi 33 kwenye Klabu Bingwa uwanjani Camp Nou ikiwemo kubwaga Inter mara mbili.