Michezo

Hali tete Barcelona wanasoka saba wakiomba kubanduka Nou Camp

May 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

MWEZI mmoja baada ya wanachama sita wa Bodi ya Usimamizi ya Barcelona kujiuzulu, hali inaendelea kuwa mbaya zaidi kambini mwa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya soka ya Uhispania (La Liga).

Hii ni baada ya baadhi ya wachezaji kumweleza kocha Quique Setien na Rais Josep Bartomeu Maria kwamba hawajaridhishwa kabisa na namna ambavyo klabu hiyo inaendeshwa.

Miongoni mwa wachezaji hao ni beki Clement Lenglet, 24, ambaye amekiri kwamba ni wanasoka wachache sana kwa sasa wanaofahamu mustakabali wao kambini mwa Barcelona.

“Hali inatisha Barcelona. Hakuna mchezaji aliye na uhakika kuhusu kesho yake kitaaluma. Huu ni wakati mbaya zaidi kwa yeyote asiye na jina kubwa la kutajika katika ulingo wa soka kusakatia Barcelona,” akatanguliza Lenglet katika mahojiano yake na kituo cha habari cha RMC nchini Ufaransa.

“Sioni nikiendelea kuvalia jezi za Barcelona msimu ujao. Pengine hali ikibadilika, japo sioni uwezekano huo ukisalia kuwa mkubwa,” akasema.

Japo Lenglet ameridhisha zaidi kambini mwa Barcelona katika jumla ya mechi 29 zilizopita, amesisitiza kwamba atakuwa mwepesi zaidi wa kubanduka ugani Nou Camp iwapo ofa ya kuvutia zaidi itamjia.

Kwa mujibu wa magazeti mengi nchini Uhispania, ni wachezaji Marc-Andre ter Stegen, Gerard Pique, Frenkie de Jong, Antoine Griezmann, Lionel Messi na Ansu Fati pekee ndio walio na mustakabali ulio na matumaini tele kambini mwa Barcelona.

Mbali na Lenglet, wengine ambao wamefichua maazimio ya kuagana rasmi na Barcelona baada ya kulalamikia mazingira mabaya ya kufanyia kazi ni Ivan Rakitic, Arturo Vidal na Jean-Clair Todibo.

Mwanzoni mwa wiki hii, gazeti la Mundo Deportivo nchini Uhispania liliripoti kwamba Barcelona wako radhi kuwatia mnadani wanasoka saba mwishoni mwa muhula huu wakiwemo Rafinha, Rakitic, Vidal, Nelson Semedo, Junior Firpo, Todibo na Samuel Umtiti anayehusishwa pakubwa na Arsenal na Manchester United.

Kwa upande wake, Messi amekanusha kupitia mitandao ya kijamii ripoti zinazomhusisha na mpango wa kuhamia Inter Milan ya Italia.

Tetesi kuhusu uhamisho wa Messi zilishika kasi mnamo Ijumaa baada ya nahodha huyo kufichua kwamba “anashangazwa” na migogoro inayoendelea kwa sasa kambini mwa Barcelona.

Mbali na Emili Rousaud na Enrique Tombas waliowahi kushikilia wadhifa wa urais wa Barcelona, wanachama wengine wa Bodi waliojiuzulu ni wakurugenzi wanne wakiwemo Silvio Elias, Josep Pont, Jordi Calsamiglia na Maria Teixidor.

“Tumeifikia hatua hii kwa sababu hatuwezi kubadilisha jinsi Barcelona inavyoendeshwa kwa sasa wakati ambapo kikosi kinakabiliwa na changamoto za kila sampuli,” ikasema sehemu ya barua hiyo ambayo pia ilitaka Kamati Kuu ya Barcelona kufutilia mbali bodi nzima iliyopo kwa sasa na kuagiza uchaguzi mpya wa urais.

Katika barua yao kwa usimamizi, sita hao waliangazia pia jinsi Barcelona inavyokosa mpango madhubuti wa kukabiliana na athari za kifedha zitakazotokana na virusi vya homa kali ya corona.

Awali, Messi alikuwa pia amekshifu kitendo cha Barcelona kuvutana na kampuni inayosemekana kuwachamba vikali wachezaji wa sasa na wa zamani wa kikosi hicho kupitia mitandao ya kijamii.

Hali hiyo iliyochochea Barcelona kukatiza kandarasi yake na kampuni ya 13 Ventures iliyokuwa imepatiwa kazi ya kuvumisha sifa za Bartomeu na bodi ya klabu hiyo mitandaoni.

Kwa mujibu wa redio ya Cadena Ser Catalunya nchini Uhispania, 13 Ventures ilisimamia akaunti ya Barcagate iliyokuwa ikiwakosoa mara kwa mara wachezaji Messi, Gerard Pique, Xavi Hernandez, Pep Guardiola na Carles Puyol kwenye mitandao ya kijamii ya Facebook na Twitter.

Miongoni mwa jumbe zilizotajwa na ripoti hiyo ni moja iliyotoa hisia kali dhidi ya straika Messi kuchelewa kusaini kandarasi mpya. Ujumbe mwingine ulipinga Pique kujihusisha na mashindano ya tenisi ya Davis Cup.

Messi ameshikilia kwamba itakuwa vigumu zaidi kwa Barcelona kutia kapuni ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika misimu ya hivi karibuni iwapo mizozano inayoshuhudiwa kwa sasa ugani Nou Camp itaendelea.