Michezo

Harambee Stars kuvaana na Gambia Alhamisi kabla ya kupepetana Gabon ugani Nyayo

Na JOHN ASHIHUNDU March 17th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KOCHA wa Harambee Stars, Benni McCarthy ametaja kikosi cha wachezaji 23 kitakachopambana na Gambia na baadaye Gabon kwenye mechi ya mchujo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2026.

Kikosi hicho kitaanzia ugenini Alhamisi (Machi 20) dhidi ya Gambia ugani Stade Allasane Quattara nchini Ivory Coast kabla ya kurejea nchini kualika Gabon mnamo Jumapili (Machi 23), ugani Nyayo kuanzia saa kumi jioni.

Wachezaji hao ni pamoja na Farouk Shikalo, Rooney Onyango, Manzur Okwaro, Ben Stanley Omondi na Mohammed Bajaber wanaosakatia klabu za nyumbani.

Akitaja kikosi hicho, McCarthy hakumshirikisha William Lenkupae, Mkenya aliyezaliwa nchini Australia, licha ya uchezaji wake kuvutia Wakenya wengi wanaomfuatilia.

Staa mwingine aliyetemwa kutoka kwa kikosi cha muda ni kiungo Austin Odhiambo ambaye amekuwa na kiwango kizuri akichezea Gor Mahia kwenye Ligi Kuu Nchini (FKF-PL).

Wengine waliochujwa ni Sylvester Owino, Alphonce Omija, Lawrence Juma na Alpha Onyango, huku wachezaji kadhaa wenye ujuzi wa kutosha wakijumuishwa.

Harambee Stars inakamata nafasi ya nne katika Kundi F baada ya kujikusanyia pointi tano, kufuatia ushindi mmoja dhidi ya Uchelicheli, sare mbili dhidi ya Burundi na Ivory Coast wanaongoza kundi hilo kwa pointi 10.

Makipa ni: Ian Otieno, Brian Bwire na Faruk Shikhalo.

Walinzi: Jonstone Omurwa, Brian Mandela, Daniel Anyembe, Amos Nondi, Erick Ouma, Manzur Okwaro na Ronny Onyango.

Viungo: Anthony Akumu, Richard Odada, Ismael Gonzalez, Timothy Ouma, Eric Johana, Duke Abuya, Mohammed Bajaber na Ben Stanley Omondi.

Washambuliaji: Masud Juma, Jonah Ayunga, Elvis Rupia, John Avire na Michael Olunga.