• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 10:44 AM
Harambee Stars yaahidi burudani isiyo kifani Afcon

Harambee Stars yaahidi burudani isiyo kifani Afcon

Na GEOFFREY ANENE

KIUNGO wa Harambee Stars, Dennis Odhiambo amepuuzilia mbali kwamba Kenya itakuwa ikisindikiza timu zingine katika Kombe la Afrika (AFCON) litakalofanyika nchini Misri kutoka Juni 21 hadi Julai 19, 2019.

Vijana wa kocha Sebastien Migne wataanza kampeni yao ya AFCON na mechi ya Kundi C dhidi ya Desert Warriors ya Algeria mnamo Juni 23, wapepetane na majirani Taifa Stars ya Tanzania hapo Juni 27 na kukamilisha mechi za makundi dhidi ya Teranga Lions ya Senegal mnamo Julai 1 jijini Cairo.

Kenya, ambayo inarejea katika kindumbwendumbwe hiki tangu mwaka 2004, itapimana nguvu dhidi ya Barea ya Madagascar mnamo Juni 7 jijini Paris nchini Ufaransa na The Leopards ya Jamhuri mnamo Juni 15 jijini Madrid nchini Uhispania kabla ya kuelekea Misri mnamo Juni 19.

Licha ya kuwa katika kundi moja na miamba Senegal na Algeria, Odhiambo anaamini kwamba Kenya imeimarika na inaweza kuandikisha matokeo mazuri katika mashindano makubwa.

“Sisi si hatupigiwi upatu kutwaa taji, lakini tumejitahidi kufika mahali tupo wakati huu na tutajaribu kufanya kila tuwezalo kuweka tabasamu katika nyuso za mashabiki wetu,” alisema Odhiambo

“Kutajwa kujiunga na timu ya taifa ni motisha kubwa na ningependa kushukuru serikali na Shirikisho la Soka la Kenya kwa kuona umuhimu kutupa muda mzuri wa kufanyia mashindano haya mazoezi ya kutosha,” aliongeza nyota huyu wa Sofapaka.

Beki

Odhiambo ni mmoja wa mabeki watano waliojumuishwa katika kikosi ambacho tayari kimekuwa na vipindi vinne vya mazoezi katika uwanja wa raga wa Marcoussis Cedex.

Mzawa wa Zimbabwe Christopher Mbamba, ambaye babake ni Mnamibia na mamake Mkenya na amewahi kuchezea timu ya chipukizi ya Uswidi, ndiye mchezaji wa hivi punde kuwasili kambini jijini Paris.

Mbamba, ambaye anasakata soka yake nchini Uswidi, ni mmoja wa wachezaji 18 kati ya 27 walioitwa, waliofika kambini.

Wachezaji Victor Wanyama, Michael Olunga, Ayub Timbe, Ovella Ochieng, Eric Johanna, Eric Ouma, Brian Mandela na makipa Patrick Matasi, John Oyemba na Faruk Shikalo wanatarajiwa wakati wowote juma hili.

Madagascar, ambayo inatiwa makali na Mfaransa Nicolas Dupuis, tayari imeshasakata mechi yake ya kwanza ya kujiandalia AFCON pale ilipolazimisha sare ya 3-3 dhidi ya wenyeji Luxembourg mnamo Juni 2.

Ilipata mabao yake kutoka kwa Paulin Voavy dakika ya 35, nahodha Faneva Ima Andriatsima (37, penalti) na Carolus Andriamatsinoro (62) nayo Luxembourg ikaona lango kupitia kwa Vincent Thill dakika ya pili, Vahid Selimovic (90+1) na Laurent Jans (90+2).

Kenya na Madagascar zilikutana mara ya mwisho miaka 20 iliyopita. Zimewahi kukutana mara 10, Madagascar ikijivunia ushindi mara tano, kupoteza mara tatu na kutoka sare mara mbili.

You can share this post!

HANG’OKI! Liverpool kurefusha mkataba wa Klopp

Mume, mke wafikishwa mahakamani wakidaiwa kuua mtoto wao...

adminleo