Harambee Stars yaangusha Chipolopolo ya Zambia kirafiki
Na CHRIS ADUNGO
HARAMBEE Stars ya Kenya iliwapiga Chipolopolo ya Zambia 2-1 katika mechi ya kirafiki iliyowakutanisha uwanjani Nyayo, Nairobi mnamo Oktoba 9, 2020.
Mechi hiyo haikuhudhuriwa na mashabiki kwa mujibu wa kanuni za Wizara ya Afya katika kukabiliana na maambukizi zaidi ya virusi vya corona.
Beki Tandi Mwape alijifunga katika dakika ya 21 ka kuwapa Stars bao la kwanza kabla ya Cliff Nyakeya kufungia Stars goli la pili kunako dakika ya 27. Goli hilo la Nyakeya anayechezea FC Masr ya Misri, lilikuwa zao la ushirikiano mkubwa kati yake na kiungo Kenneth Muguna wa Gor Mahia.
Kelvin Kampamba aliwarejesha Zambia mchezoni katika dakika ya 81 baada ya kukamilisha kwa ustadi krosi aliyopokezwa na Mwape.
Bao hilo liliwapa Zambia motisha tele na wakakita kwenye lango la Stars ambao walitegemea pakubwa huduma za wanasoka wanaochezea katika mataifa ya kigeni.
Kulishuhudiwa kizaazaa mwishoni mwa kipindi cha pili katika mchuano huo baada ya wachezaji wa Zambia kulalamikia refa Anthony Ogwayo kwa maamuzi ya kufutilia mbali bao ambalo kwa mujibu wao lilikuwa la kusawazisha.
Japo mpira ulionekana kuvuka mstari wa goli la Kenya, msaidizi wa refa aliinua kibendera chake kuashiria kwamba bao hilo lilifungwa wakati ambapo fowadi wa Zambia alikuwa ameotea.
Kocha Francis Kimanzi aliwaondoa kikosini wanasoka Masoud Juma, Kenneth Muguna na Eric Johanna Omondi katika kipindi cha pili na nafasi zao kutwaliwa na Timothy Otieno, Francis Kahata na Hassan Abdallah mtawalia.
Ushindi uliosajiliwa na Kenya dhidi ya Zambia sasa unatarajiwa kuwapa ari zaidi kadri wanavyozidi kujiandaa kwa mechi mbili za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2021 dhidi ya Comoros.
Hii ni baada ya Rais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF), Nick Mwendwa kuthibitisha kwamba Stars hawatashiriki mchuano mwingine wowote wa kujipima nguvu kabla ya kushuka dimbani kumenyana na Comoros mwezi ujao.
Stars walianza kampeni zao za kufuzu kwa fainali zijazo za AFCON dhidi ya Misri kwa sare ya 1-1 mnamo Novemba 14, 2019 ugenini kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Togo mnamo Novemba 18, 2019 jijini Nairobi.
Stars walikosa huduma za kipa Arnold Origi, kiungo Eric Johanna, fowadi Michael Olunga na nahodha Victor Wanyama katika mechi ya jana ya kirafiki dhidi ya Zambia waliotawazwa mabingwa wa AFCON mnamo 2012.
Licha ya Kenya kuvuna ushindi dhidi ya Zambia, ni wageni ndio waliomiliki asilimia kubwa ya mpira na kuonekana kuwalemea wapinzani wao katika takriban kila idara.