Michezo

Harambee Stars yapewa Tanzania, Djibouti Cecafa

November 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA watetezi Harambee Stars watapata fursa ya kulipiza kisasi dhidi ya Tanzania mapema baada ya kutiwa katika Kundi C la soka ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa Senior Challenge Cup) ya wanaume itakayofanyika Uganda hapo Desemba 7-19.

Stars ya kocha Francis Kimanzi ilizidiwa maarifa na Tanzania kwa njia ya penalti 4-1 ikibanduliwa nje ya mechi za kufuzu kushiriki mashindano ya Afrika ya wanasoka wanaocheza katika mataifa (CHAN).

Katika droo iliyofanywa jijini Dar es Salaam mnamo Novemba 24, mabingwa mara saba Kenya watalimana na washindi wa Cecafa mwaka 1974, 1994 na 2010 Tanzania, Djibouti iliyoshiriki mashindano haya mara ya mwisho mwaka 2015 na wafalme wa mwaka 1995 Zanzibar katika kundi hilo.

Kenya, Tanzania na Zanzibar pia zilikutana katika mechi za makundi mashindano haya yalipofanyika mara ya mwisho mwaka 2017. Stars ilikabwa 0-0 dhidi ya Zanzibar na kuchapa Tanzania 1-0 katika awamu hiyo kabla ya kupiga Zanzibar tena katika fainali kwa njia ya penalti 3-2 baada ya muda wa kawaida kumalizika 2-2.

Linaonekana kuwa kundi rahisi kwa Kenya, ingawa hata Djibouti haiwezi kupuuzwa baada ya kutoa Gambia jasho mwezi Oktoba katika mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (Afcon) 2021 kabla ya kubanduliwa nje kwa njia ya penalti 3-2.

Mataji mengi

Kundi A linajumuisha washikilizi wa mataji mengi ya Cecafa Uganda (wenyeji) pamoja na Burundi, mabingwa wa mwaka 1987, 2001, 2004 na 2005 Ethiopia na Eritrea inayorejea baada ya kukosa makala mawili yaliyopita.

Wageni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, washindi wa mwaka 1980, 2006 na 2007 Sudan pamoja na Sudan Kusini na Somalia iliyoshiriki mashindano haya mara ya mwisho mwaka 2015, zinaunda Kundi B.

Kutoka orodha ya washiriki, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ndio inaorodheshwa juu kwenye viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) katika nafasi ya 54. Inafuatiwa na Uganda (79), Kenya (108), Sudan (128), Tanzania (133), Burundi (143), Ethiopia (151), Sudan Kusini (162), Djibouti (185), Somalia (198) na Eritrea (206).