Hatima ya EPL msimu huu kujulikana kesho Jumatano kupitia kura
Na CHRIS ADUNGO
MIKAKATI ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kurejea inaendelea kushika kasi huku klabu za kipute hicho zikiratibiwa kupiga kura siku ya Jumatano ya Mei 27, 2020, kubaini iwapo wachezaji watarejelea mazoezi ya pamoja kambini.
Hatua hii ni njia iliyotokea baada ya Serikali ya Uingereza kulegeza kamba kwa baadhi ya kanuni zilizowekwa ili kufungua sekta ya michezo nchini humo.
Hapo jana, mwongozo unaoruhusu wachezaji kukabiliana kwa karibu wanapokuwa mazoezini ulichapishwa kwa ushirikiana na maafisa wa afya ya umma na maafisa wa soka nchini Uingereza.
Iwapo kura hiyo ya Jumatano itafaulu, itakuwa hatua ya tatu kati ya tano zilizowekwa kuhakikisha kwamba mechi za EPL zinarejelewa wakati wowote kuanzia Juni 12, 2020.
Ingawa hivyo, zipo hisia tofauti miongoni mwa washiriki wa kipute hicho ambao wanataka tarehe ya Juni 12, 2020 ambayo soka ya Uingereza inatarajiwa kurejelewa kusogezwa mbele zaidi hadi janga la corona litakapodhibitiwa kwa asilimia kubwa kote duniani.
Maamuzi muhimu kuhusu jinsi ambavyo kampeni za EPL zitarejelewa chini ya mwongozo wa masharti makali ya afya yanatarajiwa kutolewa pia asubuhi ya Jumatano katika mkutano utakaohusisha wasimamizi wa klabu zote 20 za ligi hiyo.
Iwapo pendekezo la kuanza upya kwa soka ya EPL mnamo Juni 12 litaidhinishwa, basi wachezaji wataruhusiwa kushiriki mazoezi ya pamoja katika kambi zao kuanzia Alhamisi.
Ingawa hivyo, watatakiwa kudumisha umbali wa hadi mita moja na nusu kati yao na kuzingatia kanuni zote zilizopo katika juhudi za kukabiliana ugonjwa wa Covid-19.
Kati ya masharti hayo ni kila mchezaji kufika ugani akijiendesha kwa gari lake huku akiwa tayari amevalia jezi za kujifanyia mazoezi.
Takriban klabu 14 kati ya 20 za EPL zinatakiwa kupiga kura ya ‘Ndio’; yaani kuafikiana kwamba mwongozo wa kanuni mpya za afya zitakazotolewa na maafisa wa afya kwa ushirikiano na serikali na vinara wa soka ya Uingereza utakuwa salama kwa washikadau wa mchezo huo.