Michezo

Hatima ya Man City kucheza UEFA kujulikana Julai

June 12th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na CHRIS ADUNGO

MAHAKAMA ya Mizozo ya Spoti Duniani (CAS) inatarajiwa kutangaza maamuzi ya kesi ya rufaa ya Manchester City dhidi ya marufuku ya kusalia nje ya kipute cha Uefa mnamo Julai 2020.

Mawakili watatu wa CAS sasa wana muda wa mwezi mmoja kutathmini mawasilisho yaliyotolewa kwa siku tatu zilizopita na Man-City dhidi ya vinara wa Shirikisho la soka la bara Ulaya (Uefa).

Kesi hiyo ilisikilizwa kupitia video kuanzia Juni 8-10, 2020.

“Pande zote husika zimeelezea kuridhishwa na jinsi kesi hiyo ilivyosikilizwa na sasa tunatazamia kutoa maamuzi katikati ya Julai,” ikasema sehemu ya taarifa ya CAS.

Mnamo Februari 14, 2020, Kitengo cha Uefa cha kudhibiti matumizi ya fedha miongoni mwa klabu za bara Ulaya (CFCB) kilipiga Man-City faini ya Sh3.5 bilioni baada kupatikana na hatia ya kukiuka sheria za Uefa zinazohusiana na masuala ya matumizi ya fedha (FFP) kati ya 2012 na 2016.

CFCB pia walishikilia kwamba Man-City walikosa kushirikiana vilivyo na vinara wa Uefa waliokuwa wakiwachunguza kuhusiana na kesi hiyo. Haya ni madai ambayo Afisa Mkuu Mtendaji wa Man-City, Ferran Soriano aliyakana.